Loading...

TANZIA: Msanii mkongwe wa muziki wa dansi nchini, Babu Aladini afariki dunia

Msanii mkongwe nchini ambaye ameibua na kulea vipaji vingi katika muziki wa dansi, Babu Aladini amefariki dunia, imeelezwa.

Aladini mwenye umri wa miaka 60, alifariki juzi na kuzikwa jana katika makaburi ya Kola mkoani Morogoro.

Kwa mujibu wa mdogo wa marehemu, Kulwa Milonge, ambaye ni Katibu Mkuu wa CCM Morogoro Mjini, Aladini aliugua kwa muda mrefu ugonjwa wa kiharusi kabla ya umauti kumkuta.

Alisema, kaka yake wakati wa uhai wake alimiliki bendi ya Sola Tv, ambayo wanamuziki wengi walipitia ili kuendeleza vipaji vyao na baadae kung’ara katika makundi mbalimbali ya muziki wa dansi.

Aladini alikuwa mahiri katika kuimba na kupuliza saxophone, ambapo bendi yake hiyo baada ya kuianzisha Morogoro baadaye aliihamishia Kigogo, jijini Dar es Salaam ambako yako maskani yake hadi sasa. Milonge alisema ameacha mjane na watoto watano.

Baadhi ya wanamuziki nyota waliowahi kupitia katika mikono ya Aladini ni Abuu Semhando (sasa marehemu), Shaban Lendi, Fredy Benjamin na wengine wengi.

Naye mpiga saxophone mahiri, Ally Mohamed alisema wamempoteza mwalimu na mwanamuziki mahiri katika muziki wa dansi hapa nchini na wataendelea kumkumbuka.

Aladini alikuwa akiwapokea wanamuziki chipukizi kutoka Morogoro na kuwalea kabla ya kutua katika bendi zingine, ambako walikuwa waking’ara.

Source: Habari Leo
ZeroDegree.
TANZIA: Msanii mkongwe wa muziki wa dansi nchini, Babu Aladini afariki dunia TANZIA: Msanii mkongwe wa muziki wa dansi nchini, Babu Aladini afariki dunia Reviewed by Zero Degree on 1/24/2017 11:29:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.