Loading...

Wabunge waitaka serikali kupunguza kodi

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Mazingira na Biashara imeitaka serikali kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji na wenye viwanda, ikiwemo kuondoa mlolongo wa kodi na tozo mbalimbali ambazo zimekuwa kikwazo cha kuendesha viwanda nchini.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Dalaly Kafumu ametoa ushauri huo wakati watendaji wa wizara walipokutana na kamati yake.



Dk Kafumu amesema kumekuwa na mlolongo wa kodi na tozo mbalimbali ambazo mwekezaji anatakiwa kuzilipa, na kutokana na hali hiyo wawekezaji hushindwa kuviendesha viwanda au hata kubadilisha matumizi ya viwanda hivyo, huku wengine wakikopa fedha nyingi benki kwa kutumia hati.

Ameitaka Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuonesha kwa dhati kama wanataka kuingiza nchi katika nchi ya viwanda. Mbunge wa Viti Maalumu, Anatropia Theonest (Chadema) alisema,

“Viwanda vina tozo zaidi ya 23, tuna wasiwasi tunakokwenda hata viwanda vinavyoanzishwa vitakufa kama chimbuko lililofanya viwanda vingi vishindwe kufanya kazi miaka ya nyuma”.

Mbunge wa Konde, Ally Khatibu(CUF) ametaka kuchukuliwa kwa hatua madhubuti katika kuendeleza na kuangalia matatizo ya viwanda nchini.

“Kama hatua madhubuti hazitachukuliwa tutarudi tulikotoka, sioni ishara njema tuendako,” amesema.

Mbunge wa Singida Mjini, Mussa Sima (CCM) ameitaka serikali ijiandae vya kutosha hasa pale inapoamua kuchukua kiwanda.

“Serikali ina asilimia 49 ya hisa kwenye kiwanda cha nguo cha Urafiki na mwekezaji na asilimia 51, lakini hata hivyo ufanisi wa kiwanda hicho si mkubwa sana,” amesema.

Awali akitoa taarifa ya Wizara Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk Adelhem Meru alisema serikali imefanya tathmini kwenye viwanda 80 kati ya 143 vilivyobinafsishwa na baada ya tathmini hiyo kuna baadhi ya viwanda vimefungwa.

Amesema pia baadhi ya viwanda vimehujumiwa na tathmini ya ufuatiliaji wa viwanda ilibainisha kuwa kuna wawekezaji ambao baada ya kukabidhiwa mali za viwanda badala ya kuviendeleza walihamisha mali na kuzitumia kwa matumizi mengine tofauti na yaliyokubaliwa ya uzalishaji.

A,esema baadhi ya viwanda ambavyo kwa sasa kuna kusudio la kutwaliwa kuwa ni pamoja na kiwanda cha Chuma, mgodi wa Pugu Kaolin, Mkata Saw Mills Ltd, Manawa Ginnery, Kiwanda cha Korosho Lindi, Kiwanda cha Korosho Newala, Kiwanda cha Tembo Chipboards Ltd na Kiwanda cha Mang’ula Mechanical and Machine Tools Co. Ltd.

Source: Habari Leo
ZeroDegree.
Wabunge waitaka serikali kupunguza kodi Wabunge waitaka serikali kupunguza kodi Reviewed by Zero Degree on 1/27/2017 11:58:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.