Loading...

Zaidi ya 40,000 wajitokeza kulipa madeni yao Bodi ya Mikopo

BODI ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imethibitisha kupokea malipo kutoka kwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu wa miaka ya nyuma.

Hadi kufikia jana, jumla ya wanufaika 45,000 walianza kulipa.

Wadaiwa hao wameibuka ikiwa ni siku saba tu, tangu bodi hiyo itangaze kiama kwa wadaiwa wote sugu wa walionufaika na mikopo ya bodi hiyo, ikiwa ni pamoja na kuanza kuchapisha majina na picha za wadaiwa hao kwenye vyombo vya habari.

Aidha, Bodi hiyo imeanza rasmi kuwabana waajiri wasiotimiza wajibu wao kisheria, kwa kuwatembelea kwenye ofisi zao kwa ajili ya kukagua na kuwahakiki ili kuweza kubaini, kama wamewasilisha makato na majina ya waajiriwa waliokopa HESLB.

Kwa mujibu wa Sheria mpya ya Bodi ya Mikopo, endapo waajiri hao watabaini ka kukiuka matakwa ya kuwasilisha makato na majina waajiriwa waliokopa kwenye bodi hiyo, adhabu yao itakuwa ni faini au kifungo cha miezi 36 jela.

Akizungumza kwa njia ya simu Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Abdul-Razaq Badru, alisema kwa sasa mwitikio wa wanufaika kuanza kulipa madeni yao ni mkubwa ikilinganishwa na siku za nyuma.

“Ukweli ni kwamba, mwitikio ni mkubwa, wengi wanajitokeza kulipa, wiki iliyopita tulikuwa na idadi ya wanufaika takribani 42,000 waliokuja kulipa lakini hadi leo (jana) wameongezeka na kufikia 45,000 na wanaendelea kuongezeka,” alisisitiza Badru.

Kuhusu kuanza kuchapisha majina na picha za wadaiwa wanaoendelea kutokulipa, mkurugenzi huyo alisema bado mchakato wa kutekeleza azma hiyo, unaendelea na kwa sasa bodi hiyo inafuatilia kwanza taratibu za kisheria kuhusu jambo hilo.

“Suala hili lina masuala kama mawili au matatu yanayohusu masuala ya kisheria kwa hiyo, linashughulikiwa na kitengo chetu cha sheria baada yahapo tutawaambia lini tunaanza kuchapisha majina na picha za wadau hawa sugu,” alisema.

Akizungumzia hatua ya kuwabana waajiri, Badru alisema tayari timu maalum ilishaundwa na imeanza kazi ya uhakiki katika ofisi za waajiri hao, ingawa hakutaja ofisi hizo kutokana na sababu za kiutendaji.

Katika taarifa ya salamu za mwaka mpya ziliyotolewa hivi karibuni na Ofisa Habari Mwandamizi, Elimu na Mawasiliano wa bodi hiyo, Veneranda Malima, alisema bodi hiyo iliendelea kuwakumbusha wanufaika wa mikopo waliohitimu kwenye vyuo vya elimu ya juu kuanzia miaka miwili iliyopita na kuendelea na ambao hawajaanza kurejesha, kuanza na kuendelea kurejesha mikopo yao.

“Kwa vile madeni yao yameiva muda mrefu na kugeuka kuwa wadaiwa sugu tunawataka wajitokeze kabla picha zao hazijatolewa kwenye vyombo vya habari na ambao wamo kwenye orodha ya wadaiwa sugu na tayari wamelipa benki lakini bodi haina taarifa; wawasilishe stakabadhi za malipo hayo ofisi za HESLB kwa ajili ya kuweka sawa kumbukumbu,” alisisitiza.

Tayari bodi hiyo ilishaanza kutoa majina ya wadaiwa sugu wa mikopo hiyo, ambao madeni yao yameiva lakini hawajalipa.

Hata hivyo, bodi hiyo ilitoa muda wa siku 46 kwa wadaiwa hao wajisalimishe wenyewe, ambazo ziliisha rasmi Desemba 30, mwaka jana na kutangaza rasmi sasa hatua zitakazochukuliwa baada ya siku hizo kuwani pamoja na kuchapisha picha na majina ya wadaiwa hao.

Credits: Habari Leo
ZeroDegree.
Zaidi ya 40,000 wajitokeza kulipa madeni yao Bodi ya Mikopo Zaidi ya 40,000 wajitokeza kulipa madeni yao Bodi ya Mikopo Reviewed by Zero Degree on 1/05/2017 10:23:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.