Loading...

Aliyekuwa kocha msaidizi wa Simba, Julio asema haya kuhusu mshambuliaji Laudit Mavugo

KOCHA msaidizi wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, amefichua siri ya mshambuliaji wa timu hiyo, Laudit Mavugo, kuanza kufunga mabao katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mavugo alifunga bao maridadi dhidi ya Majimaji katika mchezo wa ligi hiyo uliochezwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Majimaji, wakati Simba wakishinda mabao 3-0 baada ya kuwekwa chini na Julio.


Akizungumza na waaandishi wa habari jana, Julio alisema alikutana na Mavugo na wachezaji wengine wa Simba katika kikao maalumu kilichowahusisha nyota wa zamani wa timu hiyo, akiwamo Zamoyoni Mogella, Abas Kuka, Mtemi Ramadhani, Dua Said na kumpa ujumbe mzito.

Julio alisema alimkalisha chini Mavugo na kumwambia Simba ni timu kubwa, hivyo matokeo mazuri uwanjani kwa asilima kubwa yanamtegemea na kumtaka mshambuliaji huyo kuamini kuwa Mungu yupo kwa ajili ya kuwasaidia waliomkosea na wale wanaomcha.

“Kwenye mpira lolote linawezekana kama tunavyoamini kuwa Mungu yupo, tusichoke kumuomba kwani ukimuomba anakupa na ukiomba msamaha kama ulimkosea atakusamehe, ukitambua hilo mambo yako lazima yaende sawa,” alisema Julio.

Julio alimtaka Mavugo kutokata tamaa kutokana na kushindwa kufunga mabao kwenye michezo kadhaa ya ligi kuu na kumtaka akaze, kwani bado ana uwezo wa kuipa matokeo mazuri timu hiyo na kumsisitiza kumcha Mungu.

“Nilikaa nikamwambia kupitwa pointi moja na Yanga wasikate tamaa kwani ubingwa bado upo kwa Simba, naamini hivyo,” aliongeza Julio.

Kwa upande wa Laudit Mavugo, amemshukuru Julio kwa nasaha zake nzuri zilizomrudisha mchezoni.

Akizungumza na BINGWA, Mavugo alisema kufanya kwake vizuri kwenye mchezo dhidi ya Majimaji ya Songea kulitokana na nasaha nzito alizopewa na kocha huyo wa zamani wa Simba.

“Kabla ya mchezo alinifuata na kuongea na mimi muda mrefu huku akiniambia uwezo wa kuipa ubingwa msimu huu ninao, hivyo natakiwa nitulize akili nicheze kwa kujiamini mwisho wa siku niipe matokeo timu,” alisema Mavugo.

“Aliniambia ni mchezaji ambaye Simba inanitegemea na ubingwa wa msimu huu upo mikononi mwangu, kwa kweli maneno hayo yalinijenga na kunifanya nijiamini muda wote wa mchezo,” aliongeza Mavugo.

Alisema tangu atue Tanzania hajawahi kupata mtu na kuzungumza naye maneno muhimu kama hayo na kumfanya ajione yeye ni shujaa.

“Ukweli maneno ya Julio yamenijenga na sasa najiona jasiri, naamini nitabadilika na kufunga katika kila mechi ambayo nitapangwa kwenye kikosi cha Simba.”

Source: Bingwa
Aliyekuwa kocha msaidizi wa Simba, Julio asema haya kuhusu mshambuliaji Laudit Mavugo  Aliyekuwa kocha msaidizi wa Simba, Julio asema haya kuhusu mshambuliaji Laudit Mavugo Reviewed by Zero Degree on 2/09/2017 11:17:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.