Loading...

Mashabiki wa Klabu ya Arsenal wamgeukia Mesut Ozil

MESUT Ozil bado hajafikia maamuzi ya kuongeza mkataba wake katika kikosi chake cha Arsenal, kitu ambacho kinaendelea kuwaumiza vichwa mashabiki wake wanaotaka asiondoke.

Mkataba wa Mjerumani huyo unaenda sambamba na ule wa kocha wake Arsene Wenger, ambaye naye baada ya msimu huu kuisha mkataba wake utakuwa umemalizika hiyo ikimaanisha kuwa kikosi hicho kinatakiwa kufanya kazi ya ziada kuwasainisha.

Licha ya kwamba Ozil alisema anaweza kusaini endapo klabu yake hiyo itakubali kumlipa mshahara kiasi cha Euro 200,000 kwa wiki, ambapo wakati hilo likiwa bado linajadiliwa, mchezaji huyo aliibuka na jambo jingine.

Jambo lenyewe ni kwamba, Mjerumani huyo anataka kuhakikisha kwamba kocha wake naye atabakia katika klabu hiyo kwani ndiye aliyemwamini na kuamua kumsajili kutoka Real Madrid inayoshiriki Ligi Kuu nchini Hispania maarufu kama ‘La Liga’.

Hata hivyo, wakati Ozil akisema hatasaini mpaka atakapojua mustakabali kwa Wenger, ni kama baadhi ya mashabiki wameamua kumjibu kiaina baada ya kuibuka na mabango yakimtaka kocha huyo kuachia ngazi kwa madai kuwa mbinu zimemwishia.

Baadhi ya mashabiki hao waliibuka na mabango hayo mwishoni mwa wiki iliyopita waliposhuhudia klabu yao hiyo ikibamizwa mabao 3-1 kutoka kwa vinara wa ligi hiyo Chelsea mchezo uliochezwa Uwanja wa Stamford Bridge.

Matokeo hayo yanawafanya Arsenal kuzidi kuporomoka ambapo sasa wanashika nafasi ya nne na kama watapata matokeo mengine mabaya mwishoni mwa wiki hii dhidi ya Hull City, hali inaweza ikawa mbaya zaidi.

Arsenal walikuwa wamepewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa msimu uliopita kutokana na zile timu kubwa zote kuwa katika viwango vya chini, lakini waliwaachia njia Leicester City, wakatwaa ubingwa huo jambo ambalo halikuwafurahisha mashabiki wa washika bunduki hao.

Mashabiki hao wa Arsenal, wanakereka sana kuiona timu yao miaka nenda rudi wakigombania nafasi ya nne badala ya kupigania ubingwa na sasa wameona ni vema kocha huyo akapisha mwingine mwenye malengo tofauti na yake.

Mabango hayo ya mashabiki wanaotaka Wenger aondoke wanamaanisha kuwa hata Ozil akiondoka sawa tu, kwani waliondoka wachezaji wengi wenye majina na timu ikaendelea kubaki kama ilivyo na akija kocha mwingine atasuka kikosi cha kazi.

Hata hivyo, wakati hayo yote yakiendelea ikumbukwe kuwa hii si mara ya kwanza baadhi ya mashabiki wa Arsenal kumshinikiza Wenger kuachia ngazi, lakini mwisho wa siku anaongeza mkataba.

Hiyo inamaanisha kuwa wakati huu likiwapo shinikizo la hao wanaotaka Wenger aondoke, haitashangaza siku chache zijazo akakaa meza moja na uongozi na kuongeza mkataba mwingine kwani ndivyo wanavyofanya kila mara.

Mashabiki wa Arsenal wanakereka kuona wenzao wakitwaa ubingwa kila mara ndiyo maana wanataka aje kocha mwingine, lakini viongozi wanaridhika na kazi yake ndiyo maana hawataki kuona anaondoka.

Uzoefu unaonyesha kuwa Wenger atapewa mkataba mwingine lakini ujumbe utakuwa umemfikia Ozil kwamba mashabiki hawamtaki kocha huyo baada ya kuingia uwanjani na mabango.

Arsenal wapo nafasi ya nne kwenye msimamo wakiwa na pointi 47 na kama watapoteza mwishoni mwa wiki hii dhidi ya Hull City, wanaweza wakajikuta wanaporomoka hadi nafasi ya sita endapo Liverpool na Manchester United watashinda michezo yao.

Liverpol wanashika nafasi ya tano wakiwa na pointi 46 ambapo wakiwafunga Tottenham watafikisha pointi 49 na kama Manchester United wenye pointi 45 katika nafasi ya sita wakishinda dhidi ya Watford, watafikisha pointi 48 hiyo ikimaanisha kuwa Arsenal wanatakiwa kupambana vilivyo.
Mashabiki wa Klabu ya Arsenal wamgeukia Mesut Ozil Mashabiki wa Klabu ya Arsenal wamgeukia Mesut Ozil Reviewed by Zero Degree on 2/09/2017 11:22:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.