Loading...

Baada ya kushamiri kwa vita ya kuzui dawa za kulevya, ..'Mateja' waibuka na vilevi vipya jijini Dar

VITA ya kupambana na dawa za kulevya ikiwa imeshika kasi nchini na kusababisha kupungua kwa mihadarati sokoni baada ya wafanyabiashara hiyo kuhofia kukamatwa, watumiaji 'mateja' wameibuka na vilevi mbadala.

Uchunguzi umegundua kuwa 'mateja' ambao bado wapo mitaani baada ya watumiaji wengi kuonekana kukimbilia katika nyumba za matibabu, wamelazimika kutumia vileo mbadala ili kukidhi haja ya miili yao. 



Uchunguzi katika maeneo ya jiji la Dar es Salaam ambayo huwapo watumiaji wengi wa dawa za kulevya, umebaini kuwa 'mateja' wamehamia kwenye vileo kama mafuta ya petrol, ugoro na gundi ya viatu baada ya kukosa dawa za kulevya.

Vita dhidi ya dawa za kulevya nchini ambayo imepata msukumo mpya tangu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ataje watu 65 waliotakiwa kuisaidia polisi kuhusu biashara ya mihadarati wiki mbili zilizopita, ilipata nguvu zaidi wiki iliyopita kutoka kwa IGP, Ernest Mangu.


Kabla ya kutaja orodha hiyo iliyokuwa na viongozi wa dini, wafanyabiashara na wanasiasa, Makonda alikuwa ametoa orodha ya Polisi 12 na wasanii kadhaa ambao walitakiwa pia kufika Kituo Kikuu cha Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa mahojiano.

Tangu hapo, vita dhidi ya biashara ya mihadarati nchini imekuwa gumzo na jana IGP aliamuru katika taarifa yake Makamanda wa mikoa yote waongeze nguvu.

Zaidi ya watu 500 wamekamatwa katika mikoa mbalimbali nchini wakihusishwa kwa namna moja au nyingine na biashara ya madawa ya kulevya hivyo kupelekea 'unga' kupotea mitaani.

Wakizungumza na Nipashe katika uchunguzi huo, baadhi ya watumiaji hao walieleza kuwa kwa sasa dawa za kulevya zimekuwa adimu mitaani na upatikanaji wake ni wa taabu.

Mmoja wa watumiaji aliyejitambulisha kwa jina la Bakari Mwarabu, mkazi wa Mwanyamala alisema kwa sasa hutumia petroli kunusa kama mbadala wa dawa za kulevya.

“Ninaenda kwenye gereji ninaomba mafuta ya petroli kwa sababu sheli hawawezi kuniuzia, ninaweka kwenye kikopo ninanusa baada ya hapo ninajisikia safi kabisa,” alisema Mwarabu.

Alisema petroli inaendana na dawa za kulevya na kwamba kwa sasa ndiyo mbadala kwake.

Mtumiaji mwingine ambaye hakutaka kutaja jina lake katika maeneo ya Ubungo, alilieleza Nipashe kuwa baada ya kuadimika kwa dawa za kulevya, hutumia ugoro.

Alisema huweka ugoro huo kwenye pua "ili kujiweka sawa kiakili".

Alisema anapovuta ugoro kwa kutumia pua hupiga chafya mara kadhaa hali inayomsababishia kujisikia nafuu kidogo kuliko kutokupata 'unga' kabisa.

“Ugoro upo mwingi tu, Wamasai wapo wengi wanauza mitaani wala hakuna taabu ya kupata," alisema.

"Dawa za kulevya sasa huwezi kupata kirahisi (na) ukipata basi wewe na muuzaji mnafahamiana sana.”

Mtumiaji mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Shaka Zulu mkazi wa Magomeni alilieleza Nipashe kuwa yeye hutumia gundi ya viatu kunusa kama mbadala ya dawa za kulevya.

Alisema gundi ya viatu akiinusa mara kwa mara humsababishia kulewa na kwamba "stimu" yake inafanana na ya dawa za kulevya.
Alisema hupata gundi ya viatu kwa marafiki zake washonaji viatu ambao humwekea katika kichupa kidogo.

KAMATA KAMATA

Katika vita hiyo dhidi ya watu wanaojihusisha na madawa ya kulevya, na tangu IGP atoe agizo, makamanda wa polisi wa mikoa mbalimbali wamekuwa wakitaja orodha ndefu zinazotokana na kamata kamata.

Mkoani Dodoma, watu 168 walikamatwa na Jeshi la Polisi katika Wilaya ya Dodoma kwa kukutwa na dawa za kulevya aina ya bangi, mirungi na cocaine wiki iliyopita.

Mkuu wa wilaya hiyo, Christina Mndeme, alisema kati ya watuhumiwa hao waliokamatwa, 140 ni wanaume na wanawake ni 28.

Mkoani Lindi, watu 79 walikamatwa kwa tuhuma za makosa mbalimbali, ikiwamo kujihusisha na dawa za kulevya wiki iliyopita pia.

Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga lilitangaza kuwatia mbaroni watu 17 wanaodaiwa kujihusisha na dawa hizo katika wiki yake ya kwanza na mkoani Iringa, Jeshi hilo lilikuwa likishikilia watuhumiwa 21 katika Manispaa ya Iringa.

Watuhumiwa 47 walitajwa na kutiwa mbaroni mkoani Kilimanjaro kwa tuhuma za kujihusisha na dawa za kulevya wakati katika
Mkoa wa Mwanza mtu mmoja alikamatwa Februari 2, akituhumiwa kukutwa na dawa aina ya heroine pinchi 240 na ndogo mbili, huku Jeshi la Polisi likisema kuwa linausaka mtandao wote.

Katika Mkoa wa Dar es Salaam ambao umekuwa kitovu cha vita hiyo iliyochochewa na Makonda, orodha ya majina ya watuhumiwa 184 ilikabidhiwa na Makonda mwenyewe kwa Jeshi la Polisi na kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Sianga.

Orodha ya kwanza ya majina 22 na ya pili ya majina 65 alizikabidhi kwa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro na ya tatu ya majina 97 aliikabidhi kwa Sianga. Miongoni mwa aliowataja Makonda ni wanasiasa, viongozi wa dini na wafanyabiashara.

Kwa upande wake, Kamishna Sirro alisema kuwa jeshi hilo limeshawatia mbaroni watuhumiwa 311 na kwamba baadhi yao walikutwa wakiwa na vidhibiti vya kete za dawa hizo, akiwamo msanii Wema Sepetu ambaye ameshafikishwa mahakamani.

Aliongeza kuwa watuhumiwa 100 wanaendelea kusakwa na tangu Agnes Gerald 'Masogange' ni miongoni mwa waliokamatwa.

Source: Nipashe
Baada ya kushamiri kwa vita ya kuzui dawa za kulevya, ..'Mateja' waibuka na vilevi vipya jijini Dar Baada ya kushamiri kwa vita ya kuzui dawa za kulevya, ..'Mateja' waibuka na vilevi vipya jijini Dar Reviewed by Zero Degree on 2/20/2017 01:35:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.