Loading...

Ijue dawa ya Methadone inayotumiwa kutibu utegemezi wa dawa za kulevya

Methadone ni dawa inayotumika kutibu utegemezi wa dawa zingine za kulevya mfano; heroin, codeine, pethidine na morphine. Dawa hii hutolewa kwa kipimo maalumu chini ya usimamizi maalumu.

Methadone huzuia AROSTO na kupunguza au kuondoa utegemezi wa dawa za kulevya. Kwahiyo methadone hutolewa kama tiba na hupewa kwa wale wenye utegemezi wa dawa za kulevya. Kwa wagonjwa wa namna hii kwao ni mbadala salama wa dawa za kulevya wazotumia kama vile heroin.

Inawaweka huru kutoka kwenye kulazimika kutafuta dawa za kulevya na kuwapa fursa ya kuboresha maisha yao. Methadone hutumika kwa watu wote wenye utegemezi wa dawa za kulevya hata wajawazito wanaotumia dawa za kulevya hupewa methadone ili kumkinga motto aliyetumboni asipate utegemezi. Hadi sasa hakuna madhara ya methadone yanayojulikana kwa watoto wachanga.

Wakati mwingine methadone hutumika kutuliza maumivu makali ya muda mrefu au maumivu yanayosababishwa na magonjwa yasiyotibika. Watu wakianza kutumia tiba ya methadone, baadhi hujisikia raha iliyozidi na kujiskia kusinzia hali ambayo pia huletwa na baadi ya dawa nyingine za kulevya.

Dozi moja ya methadone hudhibiti arosto kati ya saa 24 hadi 36. Tiba ya kila siku ya methadone inaweza kuendelea bila kikomo ingawa pia inaweza kusitishwa kwa utaratibu maalumu. Iwapo itabidi kusitisha tiba ya methadone, dozi itapunguzwa taratibu kwa muda wa wiki au miezi kadhaa.

Iwapo methadone itasitishwa ghafla dalili kama tumbo kusokota, kuharisha, maumivu ya misuli na mifupa hutokea. Dalili hizi hujitokeza ndani ya siku moja hadi tatu tangu dozi ya mwisho. Na baadaye hupungua polepole ingawa dalili nyingine kama matatizo ya usingizi na hamu kali ya dawa za kulevya zinaweza kuendelea kwa miezi kadhaa.

Na ni muhimu unapopewa dawa yoyote na daktari mwingine hasa zenye kuleta usingizi ni muhimu umjulishe kuhusu matumizi ya methadone. Methadone hunywewa wakati wote. Hata hivyo mjulishe mfamasia wako au daktari wako aina ya chakula unachotumia kabla ya kunywa methadone. Methadone ni dawa yenye nguvu sana na inaweza kuwa na mwingiliano na dawa nyingine na kuleta madhara.

Mweleze mfamasia au daktari kuhusu dawa ulizo kunywa kabla ya kutumia methadone. Ni muhimu kumweleza mfamasia kama umekunywa pombe au dawa ya usingizi kwa mfano valium, fenegan au piriton maana huweza kuleta kifo kama itanywewa na methadone.

Kuchanganya dawa ya methadone na dawa nyingine za kulevya kunaweza kusababisha mwili kuzidiwa na dawa (overdose), hali ambayo inaweza kuhatarisha maisha.

Your Health, Our Concern

IMEANDALIWA NA:
FORD A. CHISANZA
Scientist/Researcher/Pharmacist
P.o.Box: 77150, Dar Es Salaam, Tanzania.
Mobile:+255 652466430/+255 684363584
Email: fordchisanza@gmail.com
Ijue dawa ya Methadone inayotumiwa kutibu utegemezi wa dawa za kulevya Ijue dawa ya Methadone inayotumiwa kutibu utegemezi wa dawa za kulevya Reviewed by Zero Degree on 2/14/2017 11:14:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.