Loading...

Tiketi za mchezo kati ya Simba na Yanga zagombewa na mashabiki, ..Serikali nayo yatoa onyo

Mashabiki wa Simba na Yanga wameanza kugombea tiketi za kushudia mechi hiyo ya watani wa jadi itakayofanyika Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika  vituo vya Buguruni na Chang’ombe ambapo mawakala walisema tiketi za Sh7,000 zinanunuliwa kwa wingi ikilinganishwa na tiketi nyingine.

“Mashabiki wengi wananunua tiketi za Sh7,000 na Sh10,000, ninaamini kufikia Ijumaa nitakuwa nimemaliza kuuza,” alisema Amir Mohammed wakala aliyekutwa eneo la Buguruni.

Meneja miradi wa Selcon, Galus Runyeta alisema tiketi za mchezo huo zimeshaanza kuuzwa hadi jana mchana tayari tiketi 10,000 zilishauzwa. “Tiketi zitauzwa hadi Ijumaa hakutakuwa na muda wa nyongeza,” alisema Runyeta.
Viingilio vya mchezo huo kwa viti vya blue ni Sh7,000, Orange 10,000, VIP B na C ni Sh20,000 na VIP A ni Sh30,000. 

Tiketi zinauzwa Buguruni, Mbagala, Ubungo Sheli, Karume, Mtoni kwa Aziz Ally. Pia, mabasi ya Abood yatasafirisha abiria kutoka Morogoro kuja Dar es Salaam na yatarudi baada ya mchezo.

Serikali yaonya:

Serikali imetoa onyo kwa mashabiki watakaofanya fujo siku hiyo.
Mkurugenzi wa michezo Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Yusuph Singo alisema wote watakaofanya fujo watachukuliwa hatua na siyo kuziadhibu klabu.

KUELEKEA mchezo wa watani wa jadi Simba na Yanga utakaochezwa Jumamosi ya wiki hii, serikali imetoa tahadhari kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhakikisha wanapanga waamuzi wazuri wenye maadili ya kutosha.

Mkurugenzi wa Michezo wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Yussuf Singo alisema jana Dar es Salaam kuwa matatizo yaliyotokea awali waamuzi walikuwa sehemu ya vurugu na kwamba ili yasijirudie wanahitaji kuchezesha kwa haki na kwa kuzingatia sheria za soka.

Mchezo wa mwisho wa ligi kuzikutanisha timu hizi kongwe Oktoba mosi mwaka jana kulitokea vurugu zilizosababishwa na mashabiki walioharibu miundombinu ya uwanja wa Taifa kwa kuvunja viti na milango baada ya kutoridhishwa na maamuzi ya mwamuzi wa mchezo huo, Martin Saanya.

Vurugu hizo zilitokea baada ya mshambuliaji wa Yanga, Amis Tambwe kushika mpira na mkono kabla ya kufunga bao la kuongoza jambo lililowakera mashabiki wa Simba waliomaliza hasira zao kwenye kung’oa viti. Mechi hiyo iliisha kwa sare ya bao 1-1.

Singo alisema michezo ni furaha, amani na upendo na kuwataka mashabiki watakaokuwepo siku hiyo kujiepusha na vurugu ya aina yoyote, kwani serikali imejipanga vizuri kiusalama kwa kufunga kamera 119 kona zote za uwanja na kwa yeyote atakayejihusisha na vitendo vya vurugu atawajibishwa.

“Mashabiki wajibu wao ni kwenda uwanjani kuzipa timu hamasa,” alisema huku akisisitiza umuhimu wa mashabiki kununua tiketi zao mapema ili kuepuka msongamano wa watu kwa wakati mmoja kwani kuwamudu ni vigumu.

Ofisa Masoko wa Selcom, Gallus Lunyeta alisema tiketi zimeshaanza kuuzwa na kuwahimiza mashabiki kununua tiketi mapema badala ya kusubiri siku ya mechi jambo linaloleta msongamano mkubwa.

Alisema mpaka sasa tayari wameshauza tiketi 10,000. Alisema kuwa wamebadili mashine kwa kuweka zile ambazo zinafanya kazi haraka hivyo, hakutakuwa na matatizo kama yaliyopita.

Alisema kwa mashabiki wa Morogoro na Pwani kuna magari ambayo hufika huko kuuza tiketi hizo hivyo itakuwa rahisi kwao kuzipata.

Ofisa Usalama wa Jeshi la Polisi kutoka TFF, Hashim Abdallah alisema wamejipanga kuhakikisha mchezo unachezwa kwa amani.

Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Boniface Wambura alisema waamuzi watatangazwa wakati wowote, kwani kuna baadhi wamekwenda nje ya nchi kuchezesha mechi watakaporudi watawataja.

Pia alisema, siku ya mechi mageti yatafunguliwa kuanzia saa tatu asubuhi.

Alitaja viingilio kuwa ni Sh 7,000 kwa viti vya kijani na bluu, viti vya machungwa ni Sh 20,000 kwa VIP B, C, na A itakuwa Sh 30,000.
Tiketi za mchezo kati ya Simba na Yanga zagombewa na mashabiki, ..Serikali nayo yatoa onyo Tiketi za mchezo kati ya Simba na Yanga zagombewa na mashabiki, ..Serikali nayo yatoa onyo Reviewed by Zero Degree on 2/21/2017 02:35:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.