Loading...

Askari wa jeshi la wananchi [JWTZ] ahukumiwa kwenda jela miaka 5 kwa kumuua askari mwenzake

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Tabora, imemhukumu askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Praiveti Yusuph Haji, kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatikana na hatia ya kumuua askari mwenzake kwa kumpiga risasi.

Haji alipatikana na kosa la kumuua askari mwenzake, Hildefonce Masanja bila kukusudia.

Hukumu hiyo ilitolewa na Jaji wa mahakama hiyo, Sam Rumanyika baada ya ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka kuthibitisha kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo.

Jaji Rumanyika alisema mahakama hiyo inatoa adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyo ili iwe fundisho kwake na kwa wengine wenye tabia kama yake.

Alisema upande wa mashtaka ulipeleka mashahidi sita ambao walithibitisha kuwa mshtakiwa alimpiga risasi askari mwenzake bila kukusudia na kufariki dunia papo hapo.

Akisoma hukumu hiyo ya takribani saa mbili, Jaji Rumanyika alisema mshtakiwa huyo alitoka Wilaya ya Kasulu akiwa amelewa na kuingia chumba cha kutunzia silaha ambako alichukua bunduki na kumpiga risasi askari mwenzake Masanja ambaye alifariki dunia.

Aidha, Jaji Rumanyika alisema mshtakiwa huyo alikamatwa na kupelekwa katika Kituo Kikuu cha Polisi na baada ya mahojiano, alipelekwa mahakamani.

Akijitetea huku akiongozwa na Wakili wa Kujitegemea, Method Kabuguzi, aliiomba mahakama hiyo impunguzie mteja wake adhabu kwa madai kuwa amekaa mahabusu kwa muda mrefu pia ana familia inayomtegemea.

Hata hivyo, Jaji Rumanyika alitupilia mbali utetezi huo na kutoa adhabu hiyo ya miaka mitano jela.

Awali, akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali, Antia Julius, alidai kuwa Novemba 23, 2009, saa 2:30 usiku katika Kambi ya Jeshi Kitambuka eneo la Manyovu, Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, mshtakiwa alimpiga risasi askari mwenzake Praiveti Hildefonce Masanja bila kukusudia na kufariki dunia.
Askari wa jeshi la wananchi [JWTZ] ahukumiwa kwenda jela miaka 5 kwa kumuua askari mwenzake Askari wa jeshi la wananchi [JWTZ] ahukumiwa kwenda jela miaka 5 kwa kumuua askari mwenzake Reviewed by Zero Degree on 3/17/2017 01:16:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.