Loading...

BreakingNews: Haya ndiyo maamuzi ya Jukwaa la Wahariri Tanzania [TEF] kuhusu RC Makonda

Baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda kuvamia ofisi za Clouds TV na kuwalazimisha watangaza wa kipindi cha Shilawadu kurusha kipindi kinachomuhusu Askofu Gwajima kikiwa hakijamaliziwa maandalizi kinyume na taaluma ya habari, Leo March 22, 2017 Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limefanya kikao cha maamuzi dhidi suala hilo.

TEF pamoja na Club ya Waaandishi wa Habari Dar es saalam (DCPC) na Umoja wa Club za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) zimepitisha maamuzi matatu ikiwemo.
  1. Kulaani vikali vitendo vya RC Paul Makonda
  2. Kutoandika na kutangaza habari zozote kuhusu Paul Makonda kwenye chombo chochote cha Habari.
  3. Kumtangaza RC Makonda kama adui wa Uhuru wa Vyombo vya Habari pamoja na yeyote atakayeshirikiana naye.
Jukwaa la Wahariri Tanzania(TEF) limeamua kwa kauli moja kutokuandika au kutangaza habari zozote zinazomhusisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

“Kuanza sasa, mikutano yake, shughuli zote anazozifanya Dar es Salaam hatutakwenda wala kuripoti chochote,” amesema Katibu wa jukwaa hilo, Neville Meena kwenye mkutano na waandishi wa habari.

Amesema kama kutakuwa na shughuli ambayo inahusisha kiongozi mwingine pamoja na Makonda, vyombo vya habari vitaripoti bila kumhusisha kwa vyovyote mkuu huyo wa mkoa wa Dar es Salaam.

“Makonda tutampa total black out ni kazi rahisi tu,” amesema.

“Hatutarajii kuona sura yake kwenye televisheni, hatutarajii kuona sura yake kwenye gazeti wala kusikia sauti yake kwenye redio,” amesisitiza.

Kwenye taarifa yake, TEF imelaani vikali kitendo cha Makonda kuvamia kituo cha Utangazaji cha Clouds Media Group usiku wa Machi 17 akiwa na askari wenye silaha.

“Tunaalani vitendo vya Makonda na atakayekiuka na kufanya kazi na Makonda, kitakachomkuta hatutamsaidia. Waandishi,wahariri wote tunakubaliana, sote tunasema halikubaliki na tunalaani vikali vitendo vya Makonda, utekelezaji agizo la kutokufanya kazi na RC Dar unaanza mara moja kwa vyombo vyote vya habari nchini, uamuzi huu unaungwa mkono na UTPC.”

“Kwa mantiki hiyo, tunamtangaza Ndugu Paul Makonda kuwa ni adui wa Uhuru wa Habari, na yeyote yule atakayeshirikiana naye katika kukandamiza uhuru wa habari nchini,” imesema taarifa hiyo ya TEF iliyoandikwa na Mwenyekiti wake, Theophil Makunga.

Unaweza kusoma kila kitu kwenye tamko hili hapa chini.


BreakingNews: Haya ndiyo maamuzi ya Jukwaa la Wahariri Tanzania [TEF] kuhusu RC Makonda BreakingNews: Haya ndiyo maamuzi ya Jukwaa la Wahariri Tanzania [TEF] kuhusu RC Makonda Reviewed by Zero Degree on 3/22/2017 12:40:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.