Loading...

Jinsi Simu za mkononi zilivyozifunika benki nchini katika huduma za kifedha

HUDUMA za fedha ukiwamo utunzaji fedha katika simu nchini umeleta mapinduzi kwa asilimia 22 kwenye sekta ya fedha, ikilinganishwa na kwenye benki ambazo kwa sasa watumiaji wake ni asilimia nane.

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya tisa ya Hali ya Uchumi wa Tanzania iliyowasilishwa jana na Benki ya Dunia (WB), yenye kichwa cha habari ‘Fedha iliyo karibu’ ikiwa na mada mahususi ya upatikanaji wa Huduma za Fedha kwa wote.

Imeeleza kuwa miamala ya simu ndiyo njia kuu inayotumiwa na Watanzania kujiwekea akiba, huku wanaohifadhi kwenye benki wakiendelea kuporomoka.

Imebainisha kuwa uhifadhi fedha kwenye simu ni asilimia 22, wanaoweka nyumbani ni asilimia 21, benki asilimia nane, kwa marafiki na wanafamilia ni asilimia mbili, kwenye vyama vya kuweka na kukopa ni asilimia moja.

Pia, waliojisajili kwenye miamala ya fedha ni asilimia 44 mwaka 2013 na 61 mwaka 2015, huku watumiaji halisi ni asilimia 91 mwaka 2013 na 92 mwaka 2015.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa ukuaji wa sekta ya fedha umechangiwa na watu binafsi wanaohifadhi fedha zao, na manufaa wanayopata ni usalama wa fedha zao na kujipatia fedha zaidi katika kununua na upatikanaji wa mahitaji muhimu.

Kwa kipindi cha 2011 hadi 2014, idadi ya Watanzania waliohifadhi fedha iliongezeka kwa asilimia 20.

Kwa upande wa miamala ya simu, kumekuwa na ongezeko kubwa ikilinganishwa na waliohifadhi benki na taasisi nyingine za fedha huku kukiwa na idadi ndogo ya watumiaji ukilinganisha na benki ikiwa ni anguko la asilimia 11.9 hadi 9.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa watumiaji wa benki wanaacha kutumia huduma za kibenki na kuweka fedha kwenye simu kiasi cha Sh. milioni 3 kwa mtu, na kupata faida ya asilimia mbili hadi tano ikilinganishwa na inayotolewa na benki ya asilimia 3.4 Desemba mwaka juzi.

Mwakilishi wa WB, Andrea Dall’olio, alisema mwishoni mwa mwaka 2015 huduma za miamala ya simu ilikuwa maarufu sana ikiwa na watumiaji asilimia 22.

Mkurugenzi wa benki hiyo katika nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia, Bella Brid, alisema kwa kipindi cha muongo mmoja mapinduzi ya huduma ya fedha kwenye simu za mkononi nchini yamewezesha kuongezeka kwa kiwango kikubwa.

‘Maendeleo yamekuwa makubwa sana na sasa huduma za fedha kwenye simu za mkononi ndiyo njia inayotumika zaidi kwa ajili ya kufanya malipo ya kielektroniki yenye gharama za chini. Zina uwezo wa kutoa huduma ambazo zinawaruhusu watu kuweka akiba na kukopa,” alisema.

Alisema mapinduzi hayo yana matokeo chanya katika kupunguza umaskini na pia yanachangia kurasimisha uchumi na kusisimua ukuaji wake.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, takribani mmoja kati ya watu wazima watatu, bado hawezi kupata huduma hizi, huku wanawake na wananchi wa maeneo ya vijijini wakiwa wamesahaulika kabisa.

Vichocheo vingine vya mapinduzi hayo ni pamoja na kuanzishwa kikamilifu na kwa haraka kwa mfumo wa Vitambulisho vya Taifa na mabadiliko kuelekea kwenye malipo ya kielektroniki kwa miamala inayohusu serikali, ikiwamo ruzuku ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf).

Aidha, ripoti imependekeza hatua za kuchukuliwa kufungulia ushindani katika sekta ya benki na kusaidia kuhakikisha muunganisho usio na matatizo baina ya huduma za fedha za kwenye simu za mkononi na huduma za fedha za kawaida.

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania BoT, Prof. Benno Ndulu, alisema miamala ya simu imekuwa kichocheo cha ukuaji wa sekta ya fedha, kwa kuwa ni rahisi kuwafikia watu maeneo ya vijijini.

Alisema benki hazijawa na matawi maeneo mengi nchini hususani vijijini, lakini zimejiunga kwenye huduma za simu za mkononi ambazo zimerahisisha kuwafikia wateja wao.

Kwa upande wake, Wakili Hawa Sinare alisema iko haja kwa serikali kuangalia viwango vya kodi wanavyotozwa wakulima baada ya kuchukua mikopo kwenye taasisi za fedha kwa kuwa kumekuwa na riba ambayo siyo rafiki.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Ineke Bussemaker, alisema wanaimarisha huduma za fedha kwa simu za mkononi ili kuwafikia Watanzania wengi vijijini na kuongeza uwekezaji kwenye sekta mbalimbali.
Jinsi Simu za mkononi zilivyozifunika benki nchini katika huduma za kifedha Jinsi Simu za mkononi zilivyozifunika benki nchini katika huduma za kifedha Reviewed by Zero Degree on 4/13/2017 12:26:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.