Loading...

Chama Cha Mapinduzi [CCM] kufanya mkutano mkuu maalumu Tarehe 12 Machi

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kinatarajia kufanya mkutano mkuu maalumu Machi 12, mwaka huu mkoani Dodoma.

Mkutano huo unakuwa wa kwanza kwa Mwenyekiti mpya wa CCM, Rais Dk. John Magufuli baada ya kupokea kijiti kutoka kwa mtangulizi wake Jakaya Kikwete.

Desemba mwaka jana, Halmashauri Kuu ya CCM Taifa chini ya mwenyekiti wake Rais Magufuli iliridhia mabadiliko makubwa ikiwemo kupunguza idadi ya vikao na wajumbe.

Desemba 12 mwaka jana aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye alisema baadhi ya mabadiliko hayo yanaanza mara moja na mengine yatasubiri mabadiliko ya katiba ya chama hicho.

Mbali na mabadiliko hayo, mkutano huo uliofanyika mwishoni mwaka jana ulimpitisha Rodrick Mpogolo kuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho (bara) akichukua nafasi ya Rajab Luhwavi ambaye aliteuliwa kuwa balozi huku Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana akiendelea na wadhifa huo kama ilivyo kwa wajumbe wengine watatu wa Sekretarieti.

Mkutano huo pia ulimpitisha aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Humphrey Polepole kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi huku Kanali Ngemela Lubinga akiteuliwa kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu (Siasa na Uhusiano wa Kimataifa), akijaza nafasi iliyoachwa wazi na Dk. Asha Rose Migiro.

Akizungumza jana na waandishi wa habari mjini Dodoma, Mpogolo alisema pamoja na mambo mengine mkutano huo utafanyika kutokana na mageuzi makubwa yanayofanyika ndani ya chama hicho.

Naibu Katibu Mkuu huyo alisema mageuzi hayo ni pamoja na kufanya marekebisho ya kanuni na katiba ya CCM.

“Mkutano huu pamoja na mambo mengine utafanya kazi yakujadili na kupitisha marekebisho ya katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la 2012, pamoja na kanuni za chama cha mapinduzi na jumuiya zake,”alisema Mpogolo.

Alisema kuwa kazi nyingine ya mkutano huo ni kupokea taarifa ya ratiba ya uchaguzi mkuu wa chama hicho na jumuiya zake utakaofanyika nchini kote mwaka huu.

“Marekebisho haya ya katiba na kanuni za CCM na jumuiya zake yanafanyika kufuatia maamuzi ya Halmashauri Kuu ya CCM iliyofanyika Desemba mwaka jana mjini Dar es Salaam,’’alisema Mpogolo.

Akizungumzia idadi ya wajumbe watakaoshiriki mkutano huo, Mpogolo alisema kuwa mpaka sasa bado hawana idadi kamili kutokana na uhakiki unaoendelea wa wajumbe hao.

“Bado uhakiki wa wajumbe unaendelea ukishakamilika tutatoa idadi kamili kwani kuna ambao wameshatangulia mbele ya haki na wengine wamehama chama,”alisema Mpogolo.

Aidha Mpogolo alisema mkutano huo utatanguliwa na mkutano wa Kamati Kuu (CC) Machi 10, 2017 na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Machi 11 mwaka huu.
Chama Cha Mapinduzi [CCM] kufanya mkutano mkuu maalumu Tarehe 12 Machi Chama Cha Mapinduzi [CCM] kufanya mkutano mkuu maalumu Tarehe 12 Machi Reviewed by Zero Degree on 3/03/2017 10:34:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.