Loading...

Edward Lowassa, Mbowe moto ni ule ule

WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Freeman Mbowe, ni miongoni mwa makada wa Chadema ambao wataanza leo ziara ya kikazi itakayohusisha vikao vya ndani katika majimbo ya Kanda ya Pwani, imeelezwa.

Taarifa inatolewa kwa vyombo vya habari na Idara ya Habari na Mawasiliano ya Chadema ilisema makada hao watakuwa viongozi wakuu wa chama, wajumbe wa kamati kuu na wabunge.

Ziara hiyo ya leo na kesho, imeelezwa, ni sehemu ya uimarishaji wa chama na maandalizi ya uchaguzi wa kanda hiyo utakaofanyika Jumapili.

“Mjumbe wa Kamati Kuu na Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa ataongoza timu katika majimbo ya Kisarawe na Kibamba," taarifa iliyotiwa saini na Tumaini Makene ilisema na kueleza zaidi:

"Mwenyekiti wa Chama Taifa, Freeman Mbowe ataongoza timu itakayofika katika majimbo ya Kibaha Mjini na Segerea."
Mbali na agenda ya ukaguzi wa chama na uchaguzi wa kanda, vikao hivyo pia vitajadili hali ya kisiasa katika maeneo husika na taifa kwa ujumla, taarifa ya Chadema ilisema.

Makamu Mwenyekiti Bara, Prof. Abdalla Safari ataongoza timu katika majimbo ya Mkuranga na Temeke, imeelezwa, wakati Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Said Issa Mohamed ataongoza timu katika Jimbo la Ubungo.

Katibu Mkuu, Dk. Vincent Mashinji ataongoza timu katika majimbo ya Kibaha Vijijini na Ukonga huku Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika akiongoza timu katika majimbo ya Bagamoyo na Mbagala, ilielezwa zaidi.

"Mjumbe wa Kamati Kuu na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye ataongoza timu katika majimbo ya Chalinze na Kinondoni," taarifa ya Chadema ilisema.

Mjumbe wa Kamati Kuu, Profesa Mwesiga Baregu ataongoza timu katika majimbo ya Kibiti na Kigamboni, ilisema taarifa.
Aidha, taarifa hiyo ilisema Mjumbe wa Kamati Kuu, Halima Mdee ataongoza timu kwenye majimbo ya Rufiji na Ilala.

Wajumbe wengine wa Kamati Kuu watakaokuwa katika ziara hiyo, imeelezwa, ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Arcado Ntagazwa, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee, Hashim Juma Issa, John Heche, Joseph Mbilinyi na Boniface Jacob.

Lowassa alikamatwa na kuhojiwa na Jeshi la Polisi katika ziara kama hiyo mkoani Geita, ikiwa ni mara ya pili kwa na Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Chadema kuonja 'adha' ya kuwa upinzani tangu alipokihama Chama Cha Mapinduzi (CCM) Agosti mwaka 2015.

Agosti 29, mwaka jana, Lowassa alikamatwa kwa mara ya kwanza na polisi tangu ajiunge na Chadema Julai 28, 2015.

Lowassa aliamua kuhama CCM baada ya jina lake kukatwa katika mchakato wa kumsaka mgombea wa kiti cha urais kupitia chama hicho, katika uchaguzi mkuu uliopita.

Source: Nipashe
Edward Lowassa, Mbowe moto ni ule ule Edward Lowassa, Mbowe moto ni ule ule Reviewed by Zero Degree on 3/16/2017 10:03:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.