Loading...

Hakuna wakuninyamanzisha, Paul Makonda

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Paul Makonda akizungumza na wadau kwenye sherehe ya kutimiza mwaka mmoja tangu kuwa Mkuu wa Mkoa jijini akiwashirikisha waathrika dawa za kulevya na viongozi wa dini.
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema hatanyamazishwa na mtu yeyote katika mapambano ya vita ya dawa za kulevya.

Alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wadau na waathirika wa dawa za kulevya kuhusu mikakati yake baada ya kufikisha mwaka mmoja akiongoza mkoa huo.

Makonda alisema kumekuwa na maneno mengi yakizungumzwa, baada ya kuanza kwa sakata la dawa kulevya, jambo ambalo linaashiria vita hiyo imewagusa wengi.

Aliongeza kuwa wapo watu waliobeza mbinu aliyoitumia katika kuwataja wafanyabiashara, watumiaji na waingizaji wa dawa hizo, lakini akasema kama wangeamua kufanya bila kuwataja, wananchi wengi wangeendelea kuangamia.

“Kwanza unatakiwa ujiulize wewe ni nani na umetoka wapi? Acha idadi ya wanaonichukia waongezeke, sina sababu ya kupendwa. Kama tungeamua kuwaita kimya kimya tukala fedha zao mngejua, kuepuka hilo ndio maana tukaamua kuwa wazi,” alisisitiza Makonda.

Aliongeza kuwa mpaka sasa wapo vijana zaidi ya 11,000 ambao wapo tayari kuachana na matumizi ya dawa za kulevya.

“Hawa ni wale ambao wamekuwa tayari na kujitokeza, lakini wapo wengi zaidi, niseme tu wewe kijana ambaye unatumia, unasambaza na unayetumika katika kutakatisha fedha lakini unaamua kufanya siri ni bora ukajitokeza, sababu kasi inayokuja sasa ni tofauti,” alisema Makonda na kuongeza kuwa, ili kuhakikisha wanadhibiti matumizi ya dawa za kulevya kuanzia chini, wataanza operesheni shuleni ili kuwasaka wanafunzi wanaotumia dawa hizo kabla ya kuingia darasani.

“Tumeambiwa wapo wanafunzi wanaotumia dawa za kulevya chooni ndipo waingie darasani, sasa kwa kuwa tumeamua kumaliza suala hili tutapita shuleni kuwasaka wote wanaojihusisha na matumizi ya dawa hizi hatari,” alisema Makonda ambaye kabla ya kuteuliwa kuwa mkuu wa mkoa huo, alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni.

Aidha, alisema ofisi yake wakishirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango, wataanzisha operesheni ya kuyapitia maduka ya kubadilishia fedha ili kujiridhisha kama yanatumika katika kutakatisha fedha za wauza dawa za kulevya.

“Wauza dawa za kulevya walianza kuyatumia maduka haya kutakatishia fedha zao baada ya kuona wakitumia njia za kibenki watakamatwa, sasa tutaanza operesheni hii kujiridhisha, hatuwezi kuwa na maduka haya ya kubadilishia fedha mengi kuliko maduka ya vocha,” alieleza.

Makonda pia alizungumzia changamoto alizokutana nazo katika kipindi cha mwaka mmoja katika uongozi wake, akieleza kwamba kumekuwa na utendaji wa mazoea kwa baadhi ya watendaji wa serikali katika kuwahudumia wananchi, jambo ambalo linasababisha kero kwa wananchi.

“Watendaji wamekuwa wakiwasumbua wananchi kwa jambo dogo sana, hali ambayo inasababisha wananchi kuamua kutafuta njia nyingine, ikiwa ni pamoja na kuleta malalamiko yao katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa hata Rais kwa kitu ambacho kinaweza kushughulikiwa na mtaa. Kwa kipindi hiki jambo hili sitaki kuliona tena,” aliongeza.

Pia alisema changamoto nyingine aliyokutana nayo ni muda wa kuwahudumia wananchi kuwa mfupi.

“Nina uhakika sijafanikisha kuonana na kila mwananchi, lakini kwa sasa nitajitahidi kwa uwezo wangu japo najua ni ngumu, lakini nitatumia njia mbalimbali kuhakikisha nawafikia wananchi na kuwasikiliza na kutatua kero zao,” alieleza.

Makonda alisema mikakati yake kwa mwaka wake wa pili madarakani ni pamoja na kuhakikisha anasimamia utendaji wa watendaji wa serikali ili kuhakikisha wanawatumikia wananchi ipasavyo, pamoja na kusimamia ipasavyo wakandarasi wanaopewa miradi katika mkoa huo, kufanya kazi ipasavyo na watakaposhindwa kufanya, watairudia kwa gharama zao pamoja na kufungiwa kufanya kazi katika mkoa huo kwa muda wa miaka mitatu.

“Nitasimamia hili kwa nguvu zote najua kuna kampuni mbili ambazo sitaki zipewe tena kazi katika mkoa wangu, Watanzania wamechoka kuwa na miradi ya kutumika kwa muda mfupi na kuharibika na nitahakikisha nawawajibisha watendaji wote watakaosindwa kusimamia miradi hiyo,” aifafanua Makonda.

Alisema ili kuhakikisha wananchi wanasikilizwa kuanzia ngazi ya chini, ataanza ziara katika ofisi za mitaa ili kuangalia utendaji wa serikali za mitaa wanavyofanya kazi.

Akizungumzia wananchi wanaoishi mabondeni, alisema atawapatia viwanja wenye hati miliki, lakini atawashughulikia wote waliohusika kutoa hati hizo.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi Simon Sirro alisema jeshi hilo limebaini kuendeshwa kwa mafunzo ya mapigano ya karate na judo pamoja na matumizi ya silaha katika baadhi ya nyumba za ibada.

Kamanda Sirro alisema mafunzo hayo, yamekuwa yakifundishwa katika nyumba hizo, ambazo ni misikiti na makanisa kwa watoto wadogo, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria na kuwaomba viongozi wa dini kuhakikisha wanakemea na kutoa taarifa kwa jeshi hilo.

“Tuna taarifa za kufanyika kwa mafunzo ya karate na judo, lakini pia watoto wadogo wa miaka mitano na sita wanafundishwa kutumia silaha, matokeo yake tutakuwa na watu ambao ni hatari kwa jamii, tunaomba viongozi wa dini mtoe ushirikiano kwa Jeshi la Polisi,” alisema Kamanda Sirro.

Naye Mbunge wa Jimbo la Ilala, Mussa Azzan Zungu alisema anaunga mkono vita dhidi ya dawa za kulevya ambayo imeanzishwa na Rais John Magufuli pamoja na Makonda.

Alisema vita ya dawa za kulevya ni lazima iwe na misukosuko, lakini ni lazima washinde, hivyo aliwataka wananchi kuunga mkono vita hiyo na sio kumuachia mkuu wa mkoa pamoja na Rais.

“Kuna watu mwanzoni walikuwa wanasuasua, lakini sasa hivi hawajapigiwa wanacheza, jitokezeni kuunga mkono juhudi hizi,” alieleza Zungu.

Source: Habari Leo
Hakuna wakuninyamanzisha, Paul Makonda Hakuna wakuninyamanzisha, Paul Makonda Reviewed by Zero Degree on 3/16/2017 01:09:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.