Loading...

Maelezo ya uongozi Yanga juu ya tetesi za Donald Ngoma na Bossou kutaka kuachana na klabu hiyo

UONGOZI wa Yanga umesikia tetesi zinazozagaa mitaani kwamba, wachezaji wao muhimu, Donald Ngoma na Vincent Bossou, wataondoka baada ya mikataba yao kumalizika, kisha wakasema haondoki mtu ng’o na badala yake wapo kwenye mikakati ya kuwaongezea mikataba mipya.

Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Clement Sanga, amesema wanatambua mikataba ya wachezaji hao inamalizika mwishoni mwa msimu huu, lakini kama viongozi, wanatarajia kukutana kwa ajili ya kujadiliana namna ya kuwaongezea mikataba mingine minono ili waendelee kuitumikia klabu hiyo.

Sanga pia ameweka wazi kwamba, kauli za kuondoka zinazodaiwa kutolewa na wachezaji wenyewe kupitia mitandao ya kijamii huwa wanaikana pale wanapoitwa na viongozi na kuulizwa kuhusu madai yao.

“Tumesikia kauli mbalimbali juu ya wachezaji hao, ila tukiwaita kuongea nao wanakataa katakata kwamba si wao, sasa tunashindwa kujua lipi ni sahihi, ila sisi tunatambua ni wachezaji wetu na tutaendelea kuwa nao,” alisema Sanga.

Kuhusu taarifa kuwa wapo baadhi ya wachezaji wanaodai mishahara, alikiri kuwa hilo lipo na kwamba wanapambana kwa kila hali kuhakikisha wanalimaliza tatizo hilo mapema iwezekanavyo.

Wakati Sanga akisema hayo, taarifa zisizo na shaka zinadai kuwa, Bossou na Ngoma wapo kwenye mipango ya kuikacha timu hiyo na kutimkia kwingine kwa lengo la kutafuta maisha mbele ya safari.

Wachezaji hao kila mmoja kwa nyakati tofauti wamehakikisha juu ya kutopenda kuendelea kuitumikia timu hiyo ya Jangwani, kwa vile wakati wanajiunga walikuwa na malengo ya kuitumikia kwa muda na kisha kujaribu kutafuta maisha maeneo mengine.

Katika hatua nyingine, baadhi ya matajiri waliokuwa wakiisaidia timu hiyo kipindi cha nyuma wametajwa kurejea kwa ajili ya kuweka mambo sawa na huenda ndio hao walioufanya uongozi kupitia Makamu Mwenyekiti kueleza nia ya kuwapa mikataba mipya wachezaji wao kutoka nje ili waendelee kuitumikia timu hiyo.

Kiongozi huyo pia aliweka wazi kwamba, matajiri wanaotajwa kurejea kundini ni Abdalah Bin Kleb na Seif Magari, ambao wapo muda wote katika klabu hiyo na wamekuwa wakitoa misaada mbalimbali, kwa hiyo hakuna wasiwasi juu ya kuwapo kwao kwasasa ili kusaidia kuweka mambo sawa.

Kwa upande wa Bin Kleb, alipoulizwa juu ya mikakati yao mipya alisema kwamba, yeye hajawahi kutoka Yanga na kwamba bado yupo katika kamati ya usajili na ataendelea kutoa misaada kadri atakavyoweza, kwa vile nafasi yake inahitaji nguvu za kiuchumi.

Klabu ya Yanga inasemekana ipo katika hali mbaya ya kiuchumi kiasi cha kushindwa kulipa mishahara ya wachezaji kwa muda muafaka, hata hivyo, Sanga alisema kwamba, hivyo ni vipindi vya mpito ambavyo vimewahi kuikumba klabu hiyo mara nyingi tangu ilipoanzishwa mwaka 1935.

Source: DIMBA
Maelezo ya uongozi Yanga juu ya tetesi za Donald Ngoma na Bossou kutaka kuachana na klabu hiyo Maelezo ya uongozi Yanga juu ya tetesi za Donald Ngoma na Bossou kutaka kuachana na klabu hiyo Reviewed by Zero Degree on 3/05/2017 02:36:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.