Loading...

Mahakama yatupilia mbali ombi la Mbowe, ...yatoa ruksa akamatwe

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetupilia mbali maombi ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe aliyoomba asikamatwe na Polisi, baada ya maombi hayo kufunguliwa kwa sheria isiyo sahihi.

Uamuzi huo umefikiwa baada ya jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Sekieti Kihiyo akisaidiana na Jaji Lugano Mwandambo na Jaji Pellagia Kaday, kuridhishwa na hoja ya Wakili Mkuu wa Serikali, Gabriel Malata ambaye aliomba mahakama isikubaliane na maombi hayo kwa kuwa yana makosa kisheria.

Katika uamuzi huo uliosomwa na Jaji Mwandambo kwa niaba ya jopo, ulisema kuwa kifungu cha sheria walichokitumia wadai hao kupitia mawakili wao, Peter Kibatala na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu hakikuiwezesha mahakama kukubaliana na maombi yao.

Katika kesi hiyo ya Kikatiba Namba 1 ya mwaka 2017, Mbowe aliwasilisha maombi yake kupinga mamlaka ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Kamanda wa Polisi Kanda hiyo, Simon Sirro na Mkuu wa Upelelezi wa kanda hiyo (ZCO), Camilius Wambura ya kutaka kumkamata hadi maombi hayo yatakaposikilizwa.

Kutokana na uamuzi huo, Jeshi la Polisi lipo huru kumkamata na kumshikilia Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai mkoani Kilimanjaro. Zuio la awali, lililotolewa na mahakama lilitaka asikamatwe na badala yake aitwe kwa mahojiano na upelelezi pindi watakapomhitaji.

Awali, katika shauri lililopita, jopo la wanasheria wa serikali likiongozwa na Malata, Paul Shaidi na Sylvester Mwakitalu, ulitoa mapingamizi kupinga maombi ya mdai yasikubaliwe mahakamani kwamba yanamakosa kisheria na yameletwa nje ya muda.

Malata alidai kuwa maombi hayo yameletwa chini ya sheria isiyotakiwa na kwamba hayana mashiko. Akizungumza nje ya mahakama kuhusu uamuzi huo, Jenerali Ulimwengu ambaye alijitokeza kwa mara ya kwanza katika kesi hiyo kama Wakili wa mdai, alidai kuwa watatafuta kifungu kingine cha sheria kitakachoendana na maombi hayo.

Ulimwengu alidai watafanya marekebisho ya maombi hayo kwa kutumia kifungu kinachoelezeka na kwamba wanaweza kufanya hivyo baada ya kusoma na kuelewa vizuri sheria zilizopo pamoja na uamuzi huo.

Hata hivyo, kesi ya msingi itatajwa Machi 8, mwaka huu ikiwa ni pamoja na kuingizwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) katika kesi hiyo kama mdaiwa.

Katika kesi ya msingi, Mbowe anaomba mahakama iwazuie wadaiwa kutekeleza azma yake ya kumtia mbaroni pia itoe amri ya kuwazuia kumkamata hadi hapo kesi hiyo ya kikatiba itakapomalizika na kwamba polisi wasiendelee na mchakato wowote dhidi yake hadi hapo kesi hiyo itakapomalizika.

Anadai kuwa sheria inayompa Mkuu wa Mkoa mamlaka ya kutoa amri ya kumkamata na kumweka ndani mtu iko kinyume cha Katiba kwa madai kuwa ilitungwa katika mazingira ambayo hapakuwa na vituo vya polisi vya kutosha.

Pia anadai kuwa kwa mazingira ya sasa sheria hiyo imeshapitwa na wakati na anaiomba mahakama itamke kuwa ni kinyume cha katiba.

Mbowe pia anadai kuwa hata kama Mkuu wa Mkoa alikuwa anatekeleza mamlaka yake kwa mujibu wa sheria hiyo, basi hakutimiza matakwa ya kisheria, ambayo ni pamoja na kutoa taarifa kwa Hakimu wa Mahakama ya Wilaya au ya Hakimu Mkazi.

Vile vile, anaiomba mahakama kama itaona kuwa Mkuu wa Mkoa alikuwa sawa kutoa amri hiyo basi imwamuru afuate matakwa ya kisheria, ikiwa ni pamoja na kulinda haki za binadamu katika kutekeleza madaraka yake hayo.

Source: Habari Leo
Mahakama yatupilia mbali ombi la Mbowe, ...yatoa ruksa akamatwe Mahakama yatupilia mbali ombi la Mbowe, ...yatoa ruksa akamatwe Reviewed by Zero Degree on 3/04/2017 04:10:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.