Loading...

Rais Magufuli amtia Waziri Muhongo 'kitanzini'

RAIS John Magufuli amesisitiza kuwa ni marufuku kampuni zinazochimba madini, kusafirisha mchanga wa dhahabu kwenda nje, kwa maelezo kuwa kitendo hicho ni wizi dhidi ya Watanzania.

Kutokana na hilo, amemwagiza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kusimamia kikamilifu agizo hilo, kuhakikisha kampuni hizo za madini hazisafirishi mchanga huo kwenda nje.

Alisema usafirishaji unaofanywa na kampuni hizo, umetoa fursa ya kuiba madini mengine yaliyoko kwenye mchanga huo na kuiacha nchi yenye rasilimali hizo, kutofaidika na madini hayo.

Aliyasema hayo baada ya kutembelea kiwanda cha Vigae cha GoodWill kilichoko wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani jana na kujionea teknolojia yenye uwezo wa kuchemsha baadhi ya malighafi hadi kufikia nyuzi joto 1,000 na kuchambua baadhi ya madini, wanayotaka kwa ajili ya utengenezaji wa vigae au marumaru.

“Watanzania tumekuwa tunaibiwa kwenye dhahabu, wanachukua mchanga wanausafirisha nje ya nchi, wakifika huko wanachambua dhahabu na mchanga unabaki huko huko. Ule ni wizi, sasa naagiza hakuna kusafirisha tena mchanga nje ya nchi, acha ukae huko huko, tutajenga kiwanda hapa hapa nchini,” alisema Rais Magufuli.

Alisema kiwanda kitakachojengwa, kitakuwa kinachambua mchanga huo kwa kutumia teknolojia aliyoiona kwenye kiwanda hicho cha GoodWill. Alisema hilo linawezekana, kwani gesi ya kuendeshea kiwanda cha namna hiyo ipo.

“Kwa kweli Watanzania tumechezewa mno, Waziri Muhongo (Profesa Sospeter) huko uliko kama unanitazama live (mubashara), nasema marufuku kusafirisha mchanga tena nje ya nchi,” alisisitiza Rais Magufuli, ambaye alipita kiwandani hapo akiwa safarini kuelekea katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Alisema Tanzania ina madini mengi; la sivyo kwa wizi unaofanywa na kampuni hizo za uwekezaji kwa muda mrefu, yangekuwa yameshakwisha, “Tushukuru Mungu ametupa madini mengi na hapa tulipo tumekalia mali na utajiri mwingi...kwa wizi huu yangekuwa yamekwisha,” alieleza Dk Magufuli. Alisema kwa kujenga kiwanda cha kuchuja huo mchanga nchini, kitasaidia nchi kupata mapato stahiki.

Aliitaka Wizara ya Nishati na Madini, kuhakikisha kwamba inatekeleza agizo hilo mara moja. Akizungumzia sababu ya kukataa Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Nchi za Ulaya na Afrika (EPA), Rais Magufuli alisema amekataa kusaini mkataba huo kwa sababu unalenga kuua viwanda vya ndani na kuneemesha viwanda vya Ulaya.

Alisema iwapo atasaini mkataba ule, ni wazi kuwa kiwanda kama hicho alichowekea jiwe la msingi jana, kitakufa na viwanda vya nje vitastawi. Aliwataka Watanzania kusimama imara ili kulinda viwanda vya ndani.

Pia alitoa mwito kwa wawekeza kuja nchini kujenga viwanda kwani serikali yake imedhamiria kuvilinda Waziri Muhongo aliwahi kunukuliwa akieleza kuwa mchanga ulikuwa unasafirishwa nje ya nchi ili kufanyiwa uchunguzi kutokana na ukosefu wa maabara zenye uwezo wa kubaini aina mbalimbali za madini nchini.

Profesa Muhongo aliwahi kusema usafirishaji huo sio wizi, bali hali hiyo inachangiwa na ukosefu wa vifaa vya kisasa vyenye uwezo wa kuchambua aina tofauti za madini. Alisisitiza kuwa si Tanzania pekee inayofanya hivyo, bali nchi nyingi zinasafirisha mchanga huo.

Mchanga huo ulikuwa unasafirishwa ili kwenda kuchambua, kwani katika migodi mingi ya dhahabu, yapo madini mengine kama shaba, fedha na kopa. Waziri huyo alisema suluhisho pekee la kutopeleka mchanga nje ni kujengwa maabara za kisasa zenye uwezo wa kufanya uchambuzi.

Maabara zilizopo kwa mujibu wa Profesa Muhongo, zina uwezo wa kubainisha dhahabu katika miamba ya madini kwa asilimia 40 hivyo ili kufikia asilimia 100 ya uchambuzi huo, asilimia 60 ya michanga itokanayo na miamba hupelekwa nje kuchambuliwa kwenye maabara za kisasa.

Baada ya kuweka jiwe la msingi la kiwanda cha Goodwill Tanzania Ceramic Limited, Rais Magufuli aliendelea na ziara yake kwa kuzungumza na wananchi wa Ikwiriri na kupokea kero zao ambapo amewaagiza Mamlaka ya Maji katika mji huo kuhakikisha mradi wa maji uliojengwa na kukamilika tangu mwaka 2015 kwa gharama ya Sh bilioni tano, unaanza kutoka maji kabla ya mwisho wa mwezi huu na pia amepiga marufuku utozaji wa ushuru kwa wafanyabiashara wadogowadogo wa mazao.

Pia amepokea kero za wananchi wa Somanga, Nangurukuru na Mchinga Moja na huko kote amewataka wananchi kufanya kazi kwa bidii ikiwemo kuzalisha mazao ya chakula cha kutosha huku akiweka bayana kuwa serikali haitatoa chakula cha msaada kwa watakaopatwa na njaa ilihali wanaweza kuzalisha chakula katika maeneo yao.

Aidha, Dk Magufuli amewaagiza viongozi wa Mkoa wa Lindi kushughulikia migogoro ya wakulima na wafugaji iliyoanza kuibuka mkoani humo, ameahidi kutoa Sh milioni 20 kusaidia ujenzi wa Zahanati ya Somanga, amewaagiza viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kujenga kituo cha mabasi cha Nangurukuru.

Pia amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Mchinga, Hamidu Bobali kuhakikisha anapeleka daktari katika Kijiji cha Mchinga Moja ili kutatua kero ya wananchi kukosa huduma ya matibabu. Leo ataendelea na ziara yake mkoani Lindi.
Rais Magufuli amtia Waziri Muhongo 'kitanzini' Rais Magufuli amtia Waziri Muhongo 'kitanzini' Reviewed by Zero Degree on 3/04/2017 03:56:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.