Loading...

Sakata la watumishi hewa sasa laigeukia Serikali

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene.
KIBAO kimeigeukia Serikali! Hivyo ndivyo mwingine anaweza kutafsiri baada ya kuwapo kwa taarifa kuwa baadhi ya watumishi walikumbwa kimakosa na panga lililowaondoa watumishi hewa wako mbioni kuiburuza serikali mahakamani.

Kwa sababu hiyo, Serikali imewataka wale wote waliokumbwa na kadhia hiyo kwa kuonekana kuwa ni watoro wakati ukweli ni kwamba walikuwa na barua halali zilizowaruhusu kwenda masomoni waache kuchukua hatua ya kwenda mahakamani bali wapeleke vielelezo vyao katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ili upatikane muafaka wa suala hilo kwa njia nyepesi ya kupata haki isiyohitaji mchakato mrefu wa kisheria.

Akifungua mkutano wa tisa wa wadau wa Mfuko wa Pensheni (LAPF) jijini Arusha jana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene, alisema serikali imebaini baada ya kazi ya uhakiki kuwa wapo watumishi waliofukuzwa kazi kimakosa kutokana na maafisa utumishi wao kudai ni watoro kazini lakini ukweli watumishi hao walipewa barua halali za kuwaruhusu kwenda masomoni.

Alisema wakati kazi hiyo ikiendelea, ilibainika kuwa mafaili ya baadhi ya watumishi waliokuwa masomoni hayakuwa na kumbukumbu yo yote inayotambulisha kuwa wapo masomoni hali ambayo ilitumiwa na maafisa utumishi kusema watumishi hao ni watoro.

“Maofisa utumishi wanafanyakazi zinazowahusu wafanyakazi wenzao. Tunzeni kumbukumbu zao…wapo wafanyakazi katika zoezi la uhakiki wamepata shida sana na wengine kufukuzwa kwa sababu mafaili yao hayakuwa na kumbukumbu muhimu za barua ya kuruhusiwa kwenda masomoni.

“Watumishi wote (walimu) waliofukuzwa kazi kwa sababu walitajwa kuwa ni watoro huku wakiwa na barua kutoka kwa mwajiri wao waje Tamisemi, nayo itawasiliana na Wizara ya Utumishi kutatua suala hilo,” alisema.

Alisema kazi ya uhakiki wa watumishi imewaathiri baadhi ya wafanyakazi kutokana na maofisa utumishi na wafanyakazi wa masjala kuficha au kutoweka kumbukumbu muhimu za barua za wafanyakazi walioruhusiwa kwenda masomoni katika mafaili yao.

“Baadhi ya maofisa utumishi wamewaumiza sana wafanyakazi wenzao katika zoezi za uhakiki kwa kupoteza nyaraka zilizowathibitisha kuwa wapo masomoni,” alisema.

Alisema hali hiyo, imewafanya watumishi hao kuhesabika kuwa ni watoro, hata pale walipoonyesha barua halali za kuruhusiwa kwenda masomoni, bado maafisa hao walikuwa wakiwajibu hawawezi kubadilisha kwa sababu zoezi hilo limepita.

Awali, katika hotuba yake, akimwakilisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Simbachawene aliipongeza LAPF na mifuko mingine ya hifadhi ya jamii kwa kuunga mkono azma ya Serikali ya kujenga uchumi wa kati ifikao 2025.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya LAPF, Profesa Faustine Bee, shirika hilo limeanza ujenzi wa Kiwanda cha Chai kilichopo Lushoto, mkoani Tanga, Kiwanda cha nyama kinachojengwa mkoani Morogoro na kiwanda cha vifaa vya hospitali kinachojengwa Shinyanga.

Alisema wanaendelea pia kubaini maeneo mengine ya uwekezaji wa viwanda.

Source: Nipashe
Sakata la watumishi hewa sasa laigeukia Serikali Sakata la watumishi hewa sasa laigeukia Serikali Reviewed by Zero Degree on 3/11/2017 09:15:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.