Loading...

Serikali kusambaza tiba ya 'mateja' nchi nzima

Dawa ya ‘methadone’.
SERIKALI imetangaza nia ya kufikisha huduma ya utoaji dawa ya ‘methadone’ kwa watu walioathirika na ulevi wa dawa za kulevya nchi nzima, ili kukabiliana na uhitaji mkubwa unaojitokeza sasa.

Hayo yalielezwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, na kwamba serikali imejipanga kuongeza dawa za ‘methadone’ kwa ajili ya kuwatibu vijana waliokuwa wanatumia dawa za kulevya.

Waziri Ummy alisema serikali inajiandaa kupanua huduma ya utoaji dawa kwa watu walioathirika na dawa za kulevya nchi nzima ili kukabiliana na uhitaji wa sasa.

Alisema dawa hizo zitaongezwa katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma hiyo kwa watu walioacha kutumia dawa za kulevya.

Akizungumza na Nipashe jana jijini Dar es Salaam, Waziri alisema serikali ina dawa za kutosha hadi mwisho wa mwaka huu.

Alitoa wito kwa wazazi pamoja na walezi wenye watoto, ndugu na jamaa walioathiriwa na dawa za kulevya, kuwapeleka vituoni humo ili waanze matibabu haraka.

Baada ya vita dhidi ya dawa hizo kutiliwa mkazo kuanzia mwezi uliopita kwa kukamatwa baadhi ya watuhumiwa pamoja na dawa hizo zikiwamo heroine na bangi, kulitangazwa kuwapo kwa uhaba wa dawa hizo mtaani na zile zilizosalia zikiuzwa kwa bei kubwa.

Kete huuzwa kwa Sh. 5,000 kutoka bei ya awali Sh. 500 au 1,000 .

Kwa mujibu wa Waziri Ummy, ongezeko la waathirika kwenye vituo vya kutolea ‘methadone’ ni changamoto inayohitaji kuongeza dawa hizo vituoni.

Aidha, alisema baada ya operesheni ya dawa za kulevya kuanza, serikali iliongeza dozi ya dawa Zanzibar kutokana na uhitaji uliokuwapo.

“Niwatoe wasiwasi wazazi na walezi ambao wanawaathirika wa dawa za kulevya nyumbani, dawa zipo , kikubwa wawapeleke vituoni ili waanze kupata huduma wasiwaache mtaani,” alisema.

Sakata la dawa za kulevya lilianza kushika kasi nchini mwezi uliopita baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuyaanika hadharani majina ya watuhumiwa wa utumiaji na wauzaji, sambamba na ukamataji wa dawa hizo zikiwamo heroine, cocaine na bangi.
Serikali kusambaza tiba ya 'mateja' nchi nzima Serikali kusambaza tiba ya 'mateja' nchi nzima Reviewed by Zero Degree on 3/05/2017 10:16:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.