Loading...

Serikali kutangaza ajira mpya kwa madaktari ifikapo mei mwaka huu

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Angela Kairuki.
SERIKALI imesema inatarajia kutangaza ajira mpya kwa madaktari mwezi Mei, mwaka huu na kuwasambaza katika maeneo mbalimbali yenye uhitaji.

Ahadi hiyo ilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Angela Kairuki jana akiwa katika ziara ya siku mbili mkoani Njombe, akifuatana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa.

Kamati hiyo ilitembelea Hospitali ya Makambako ambayo inajenga chumba cha upasuaji na wodi ya kinamama na watoto.

Waziri Kairuki alisema serikali itapeleka madaktari katika Hospitali ya Makambako kulingana na maombi yao katika ajira ambazo zitatolewa na serikali Mei.

Alisema eneo la Makambako linahitaji madaktari wa kutosha kutokana na ajali nyingi zinazosababishwa na kuwa mapitio ya magari kutoka maeneo ya mikoa ya Njombe, Ruvuma na Mbeya.

Ingawa Kairuki hakutaja idadi ya nafasi za ajira zitakazotolewa kwa madaktari, lakini wiki iliyopita,

Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Muhammad Kambi na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, walizungumzia suala la uhaba wa madaktati.

Prof. Kambi alisema idadi ya madaktari wanaohitajika nchini ni 3,510 na katika idadi hiyo, mahitaji zaidi yapo kwenye hospitali za wilaya wanakohitajika madaktari 832, za rufani (460), vituo vya afya (816), Bugando (152) na Hospitali ya Taifa Muhimbili madaktari 235.

Nyingine ni KCMC (143), hospitali za rufani za mikoa (460), madaktari 111 katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Hospitali ya Ocean Road (57), Mirembe (37), CCBRT (26) na Rufani Mbeya (106).

Naye Waziri Ummy alisema kuna upungufu wa asilimia 49 ya wataalamu wa afya hususani madaktari katika hospitali za umma, vituo vya afya na zahanati.

Ummy alisema uhaba wa madaktari unaikabili zaidi mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Kigoma, Mara, Simiyu, Kagera na Rukwa na kuwa hautokani na uchache wa madaktari, bali uwezo wa kuwaajiri wote kwa wakati mmoja. Alisema uwezo wa serikali ni kuajiri madaktari 400 kila mwaka.

Miaka michache iliyopita uwezo wa serikali wa kutoa ajira mpya kwa watumishi ulishuka na miongoni mwa sekta zilizoathirika zaidi ni afya.

Hali hiyo iliendelea baada ya Machi mwaka jana serikali kusimamisha ajira mpya, uamuzi ambao ulithibitishwa rasmi na Rais John Magufuli Juni 22 wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya kuanzishwa kwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Rais Magufuli alisema mbali na kusimamisha ajira mpya. pia upandishaji wa madaraja umesimamishwa na kuwa lengo la hatua hiyo ni kupisha uhakiki wa watumishi hewa na vyeti.

ZIARA YA KAMATI

Kamati hiyo ikiwa mjini Makambako ilitembelea majengo mawili ya upasuaji na wodi ya kinamama yanayojengwa na Halmashauri ya Njombe na kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi huo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jasson Rweikiza, alisema kutokana na juhudi zinazofanywa na Halmashauri hiyo, atakwenda kuisemea serikalini ili kuhakikisha kuwa huduma ya afya inapatikana kutokana na umuhimu wa mji wa Makambako.

Alisema kuwa mji wa Makambako una barabara nyingi ambazo zinapata ajali mara kwa mara na chumba cha upasuaji kitakuwa muhimu kwa kuwahudumia watu watakaopata ajali maeneo hayo.

“Kutokuwapo kwa chumba cha upasuaji ni kuwanyima watu haki ya kupata huduma ya afya, tutakachokifanya ni kuihimiza serikali kuharakisha ujenzi wa chumba hicho,” alisema Rweikiza.

Mbunge wa Kilolo, Venance Mwamoto, ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo, alisema wakazi wa
Makambako watarajie makubwa kwa kuwa ujenzi utahamasishwa ili ukamilike haraka.

“Kwa kuwa hospitali hii inahudumia wakazi wengi kutoka baadhi ya halmashauri za mikoa ya Iringa, Mbeya na Njombe, hospitali hii ni muhimu sana kwa jamii,” alisema Mwamoto.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Makambako, Charles Mbota, alisema inategemewa na wakazi wengi na huduma ya upasuaji wamekuwa wakiifuata katika hospitali binafsi ambako gharama ni kubwa.

“Kama huduma hiyo ikipatikana katika hospitali ya mji, watakuwa na unafuu wa gharama,” alisema Dk. Mbota.
Serikali kutangaza ajira mpya kwa madaktari ifikapo mei mwaka huu Serikali kutangaza ajira mpya kwa madaktari ifikapo mei mwaka huu Reviewed by Zero Degree on 3/28/2017 02:15:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.