Loading...

Siku 79 za Mbunge Peter Lijualikali akiwa jela

MBUNGE wa Kilombero, Peter Lijualikali (Chadema) aliyehukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Kilombero kwenda jela miezi sita bila faini, ameachiwa huru na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam baada ya kushinda rufaa yake huku akiwa amekaa gerezani kwa muda wa siku 79, ambazo ni takribani miezi mitatu.

Lijualikali (30) ambaye hukumu iliyompeleka jela ilitikisa nyanja za siasa na sekta ya sheria, aliachiwa huru jana baada ya mahakama kubaini hati ya mashtaka iliyomtia hatiani awali ilikuwa na upungufu mkubwa.

Mahakama hiyo ilimuachia huru jana baada ya kukubaliana na hoja zilizowasilishwa mahakamani hapo na mrufani aliyewakilishwa na Wakili Tundu Lissu, Fred Kiwelo na Enock Edwin.

Mwingine aliyeachiwa pamoja na Lijualikali baada ya hukumu yake kutenguliwa ni Stephano Mgata (35) aliyepewa adhabu ya kifungo cha nje cha miezi sita.

Lijualikali na mwenzake huyo, awali walitiwa hatiani kwa kosa la kufanya vurugu na kusababisha taharuki wakati wa mkutano wa uchaguzi wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mdogo wa Ifakara.

Uamuzi wa kuwaachia huru warufani hao ulitolewa na Jaji Ama-Isario Munisi, baada ya kukubaliana na hoja za warufani kwamba hati ya mashtaka dhidi yao ilikuwa na upungufu mkubwa usioweza kurekebishika katika hatua ya rufaa.

“Ushahidi uliotolewa na Jamhuri katika Mahakama ya Wilaya ya Kilombero haujitoshelezi kuweza kuwatia hatiani washtakiwa hao.

“Upungufu katika hati ya mashtaka ni mkubwa hivyo mahakama inatengua adhabu za vifungo walizopewa washtakiwa na inaamuru waachiwe huru,”alisema Jaji Munisi.

Awali Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kilombero, Timothy Lyon, aliwatia hatiani Lijualikali na mwenzake na kuwapa adhabu walizokuwa wakizitumikia.

Katika hukumu hiyo iliyotolewa Januari 11 mwaka huu, Hakimu Lyon, alisema Mahakama inawatia hatiani washtakiwa kwa makosa yaliyokuwa yakiwakabili.

Lijualikali alikuwa na kesi tatu huko nyuma ambazo alitiwa hatiani na kuhukumiwa, mahakama ilimuona ni mkosaji mzoefu hivyo kumuhukumu kwenda jela miezi sita.

Kesi ambazo mbunge huyo alitiwa hatiani na kuhukumiwa ni kesi namba 338 ya mwaka 2014, kesi namba 220 ya mwaka 2014 na kesi namba 340 ya mwaka 2014.

Mshtakiwa wa pili


Mahakama hiyo ilimwona mshtakiwa wa pili Mgata kuwa ni mkosaji wa mara ya kwanza hivyo kumuhukumu kifungo cha nje cha miezi sita na ndani ya kipindi hicho hakutakiwa kutenda kosa lolote la jinai.

Adhabu hiyo ilipingwa, kupitia mawakili wao walikata rufaa ambayo ilisajiliwa na kupewa namba 60 ya mwaka 2017, wakipinga adhabu hiyo wakiwa na sababu tano ikiwemo hati ya mashtaka ina upungufu mkubwa ambao hauwezi kurekebishika.

Walidai hati hiyo ya mashtaka ilikuwa haiendani na maelezo ya kosa, hivyo washtakiwa walitiwa hatiani kwa kitu ambacho hakipo.

Jamhuri ilikuwa ikiwakilishwa mahakamani na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi ambaye alipinga hoja hizo za rufani akidai hati ya mashtaka ilikuwa inakubalika kwa mujibu wa sheria na makosa yaliyoko yanarekebishika.

Alidai ushahidi uliotolewa Mahakama ya Kilombero ulijitosheleza kuwatia hatiani washtakiwa.

LISSU


Siku moja baada ya Lijualikali kuhukumiwa Lissu ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, alisema hukumu hiyo inatokana na vita vya kisiasa kati ya Chadema na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Lijualikali na Lema (Godbless-Arusha Mjini) kwa sasa yuko nje kwa dhamana baada ya kukaa mahabusu miezi mitatu kutokana na kunyimwa dhamana akituhumiwa kutoa lugha ya uchochezi, wote hawa ni wafungwa wa kisiasa.

“Adhabu ya kifungo bila faini imetolewa kwa sababu za kisiasa. Kwanza walimshitaki mara mbili, wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu ili wamfunge na asiweze kuendelea na kampeni. Haikuwezekana kumfunga na alishinda ubunge.

“Baadaye walimfungulia kesi ya uchaguzi Mahakama Kuu ambako nako tuliwashinda vibaya. Wamekata rufaa Mahakama ya Rufani ya Tanzania nako tutawashinda na wanajua hivyo,” alisema Lissu.

Alisema waliamua kumfunga mbunge huyo bila faini wakiamini kuwa uamuzi huo utamfanya akose sifa za kuwa mbunge.

Huku akinukuu Ibara ya 67 (2) (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Lissu alisema adhabu hiyo haina athari yoyote, kwa maelezo kuwa mtu anakosa sifa za kuwa mbunge iwapo atafungwa gerezani zaidi ya miezi sita.

“Si kifungo tu cha miezi sita, pia lazima awe amekutwa na hatia ya kosa lolote, vyovyote linavyoitwa, linaloambatana na utovu wa uaminifu.

“Adhabu ya kifungo aliyopewa Lijualikali haijazidi miezi sita. Pia kosa la kumpiga askari polisi, hata kama lingekuwa la kweli si kosa la utovu wa uaminifu,” alisema.

Source: Mtanzania
Siku 79 za Mbunge Peter Lijualikali akiwa jela Siku 79 za Mbunge Peter Lijualikali akiwa jela Reviewed by Zero Degree on 3/31/2017 10:28:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.