Loading...

Simba majaribuni tena

WAKATI timu ya Simba inashuka dimbani leo kumenyana na Mbeya City Mwenyekiti wa zamani wa Simba Hassan Dalali ameutaka uongozi wa Simba chini ya Evans Aveva kuwarudisha wanachama 72 waliowafutia uwanachama ili kuimarisha umoja ndani ya klabu hiyo.

Simba SC inaongoza Ligi Kuu kwa sasa kwa pointi zake 54 baada ya mechi 23, wakifuatiwa na mabingwa watetezi, Yanga yenye pointi 52.

Wekundu hao wa Msimbazi wanatarajiwa kushuka tena dimbani leo ikiwakaribisha Mbeya City katika mfululizo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Dalali amesema kuwa umoja na mshikamano ni muhimu na kwamba usiishie kwenye mechi yao na watani wao Yanga, ambao Simba walifanikiwa kushinda mabao 2-1 mwishoni mwa wiki iliyopita Februari 25 kipigo ambacho kinaiwewesesha Yanga hadi leo.

Amesema, haiwezekani Simba kuwa na umoja, huku viongozi wamewatenga wengine, kwa wakati huu ambapo timu inapigania ubingwa, ni muhimu kwa uongozi kufikiria upya kuwarudisha kundini wanachama wote waliowafuta.

“Nimewauliza wakina Aveva wana mpango gani wa kuwafutia makosa yao wanachama 72 wanasema mpaka wafute kesi mahakamani, mahakamani hakuna kesi toka ilipofunguliwa mwaka 2014 hawajawahi kuitwa mahakamani, kesi haijawahi kusikilizwa kwa kifupi hamna kesi.” amesema.

Wanachama 72 walifungua kesi ya kikatiba kupinga uchaguzi mkuu wa mwaka 2014 uliowaweka madarakani wakina Aveva na mwaka 2015 uongozi huo wa Aveva ukawafutia uwanachama kwa kukiuka katiba ya Simba, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), na CAF na FIFA kwa kwenda mahakamani.Kesi hiyo ilifunguliwa na wanachama watatu Said Babu, Peter Mongi na Peter Warioba.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa tawi la Mpira Pesa Masoud Hassan ‘Ustadh’ amesema kuwa kesho Jumapili kutafanyika usahili kwa wanachama 250 wa tawi hilo ambalo lina wanachama 1,000. Mpira Pesa ilikuwa maskani yake Magomeni lakini ilitimuliwa kwenye ofisi yake baada ya kukiuka masharti ikiwemo na vurugu na hivyo kutakiwa na uongozi kuwa na wanachama 250 kwa kila tawi.

“Wanachama 250 wa mwanzo ndio tutakaowahakiki na kuwapa usajili, wakitimia 250 watakaosalia wataenda kufanya usahili wao sehemu nyingine n a kufungua tawi lao la mpira pesa B.

Source: Habari Leo
Simba majaribuni tena Simba majaribuni tena Reviewed by Zero Degree on 3/04/2017 12:46:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.