Loading...

Ufafanuzi wa Mahakama ya Tanzania juu ya uteuzi wa Kaimu Jaji Mkuu

Mahakama ya Tanzania imewathibitishia wananchi kuwa itaendelea kufanya kazi zake kwa mujibu wa Katiba na Sheria na kwa jitihada kubwa bila woga, hofu, huba wala chuki kwa wadau wote kama inavyopaswa.

Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam kwa vyombo vya habari na Jaji Kiongozi, Ferdinand Wambali ilieza pia kwamba hakuna kosa la kikatiba lililofanywa na Rais John Magufuli kwa kumteua Kaimu Jaji Mkuu kama inavyopotoshwa na baadhi ya vyombo vya habari.

Rais Magufuli Januari 17, mwaka huu alimteua Profesa Ibrahim Juma kuwa Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Othman. Jaji Kiongozi alikuwa anatoa ufafanuzi wa habari iliyochapishwa katika gazeti moja la kila wiki, mwanzoni mwa wiki hii ikiwa na kichwa cha habari ‘Utata Jaji Mkuu.’

Alifafanua katika taarifa yake kwamba kichwa cha habari kilichoelezwa kwenye gazeti hilo kinatoa taswira hasi dhidi ya utendaji wa Mahakama na mchakato wa kupata Jaji Mkuu.

Akizungumzia uteuzi wa Kaimu Jaji Mkuu, Jaji Wambali alisema; “Kwanza ni vizuri ikaeleweka kuwa Mamlaka ya uteuzi inayo mamlaka chini ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano waTanzania ya 1977 kufanya uteuzi wa Kaimu Jaji Mkuu kama ilivyofanya kwa kuzingatia mazingira makuu matatu kama yalivyoelezwa kwenye Ibara ya 118 (4) (a), (b) na (c) ya Katiba.

“Hakuna shaka kuwa mazingira yaliyopelekea kuteuliwa kwa Kaimu Jaji Mkuu tarehe 17/1/2017 na kuapishwa tarehe 18/1/2017 ni kutokana na kiti cha Jaji Mkuu kuwa wazi kama ilivyoelezwa katika Ibara ya 118(4) (a) ya Katiba baada ya aliyekuwapo Mheshimiwa Jaji Mkuu Mohamed Chande Othman kustaafu baada ya kufikia umri uliowekwa kwa mujibu wa Katiba.

“Kwa msingi huo mamlaka ya uteuzi ambayo ni Rais imetekeleza wajibu wake wa awali kwa kuzingatia matakwa ya Katiba kama ilivvoelezwa katika Ibara ya 118(4) (c) kuhusu sifa za aliyeteuliwa kuwa miongoni mwa Majaji wa Mahakama ya Rufani.

“Kwa mujibu wa Katiba pia Kaimu Jaji Mkuu anapaswa kufanya kazi hiyo hadi atakapo teuliwa Jaji Mkuu kama inavyoelezwa katika Ibara ya 118 (5).”

Jaji Wambali alisema kutokana na matakwa hayo ya kikatiba, hakuna uvunjaji wowote wa Katiba kama baadhi ya watu wanavyodhani.

Alisema pia ni vizuri ikaeleweka kuwa Jaji anapoteuliwa kuwa Kaimu Jaji Mkuu anapaswa kutekeleza majukumu yote ya ofisi ya Jaji Mkuu kama yalivyoainishwa kwenye Katiba, Sheria na Kanuni mbalimbali.

“Vile vile anapaswa kufanya hivyo kwa kujiamini bila hofu kama anavyopaswa kufanya kazi ya ujaji. “Kwa msingi huo kazi za utoaji haki katika mhimili wa Mahakama ambao kwa sasa uko chini ya uongozi wa Kaimu Jaji Mkuu zinaendelea kutekelezwa nchini kama zinavyotakiwa kwa kuzingatia Katiba na sheria kupitia kwa Majaji, Mahakimu na watumishi wengine bila hofu, upandeleo au chuki kama ambavyo kiapo cha wote wanaohusika kinavyotaka,” alisema Jaji Wambali.

Aidha, alisema hakuna sababu yoyote ya wananchi na wadau wote wa Mahakama kuhofu kuwa yapo mambo ambayo yamekwama, yameyumba au yatayumba katika kipindi kinaposubiriwa uteuzi wa Jaji Mkuu.
Ufafanuzi wa Mahakama ya Tanzania juu ya uteuzi wa Kaimu Jaji Mkuu Ufafanuzi wa Mahakama ya Tanzania juu ya uteuzi wa Kaimu Jaji Mkuu Reviewed by Zero Degree on 3/25/2017 05:00:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.