Loading...

Viroba sasa vyageuka magendo kama bangi na 'unga'

POMBE za viroba sasa ni balaa! Kuanzia leo, yeyote atakayekutwa navyo anaweza kujikuta katika matatizo makubwa kama ilivyo kwa wahalifu wanaohusishwa na bangi, ‘unga’ na aina nyingine za dawa za kulevya.

Hali hiyo imefahamika kutokana na taarifa rasmi iliyotolewa na Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais jana huku pia baadhi ya makamanda wa mikoa wa Jeshi la Polisi wakiapa kuwachukulia hatua kali wale wote watakaowakamata navyo kuanzia leo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Serikali la kupiga marufuku vileo hivyo kuanzia leo.

TAARIFA YA SERIKALI

Katika taarifa iliyosambazwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa vyombo vya habari jana, Serikali ilieleza kwa kina namna ya kutekeleza mpango wa upigaji marufuku uzalishaji, uingizaji, usambazaji na matumizi ya vifungashio vya plastiki (viroba) kwa ajili ya pombe kali nchini

Ilielezwa katika taarifa hiyo kuwa baada ya Ofisi ya Makamu wa Rais kutangaza tangu Februari 20, 2017 juu ya utekelezaji wa amri ya kuzuia uuzwaji wa pombe kali kwa vifungashio vya viroba, sasa utekelezaji wa agizo hilo unaanza mara moja leo (Machi 1, 2017) na yeyote atakayekiuka atachukuliwa hatua za kisheria.

“Utekelezaji wa katazo hili utazingatia Ibara ya 8(1) (b) na 14, Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 na Kanuni zake zilizotungwa kupitia kifungu 230 (2) (f) cha sheria hiyo, na Sheria ya Leseni za Vileo Namba 28 ya mwaka 1968 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2012,” ilisema sehemu ya tarifa hiyo.

Aidha, taarifa hiyo ilieleza kuwa operesheni ya kukagua utekelezaji wa agizo la serikali la usitishaji utengenezaji, uuzaji na matumizi ya pombe zinazofungashwa kwenye vifungashio vya plastiki itaendeshwa nchini kote kuanzia tarehe ya kesho kwa kupitia Kamati za Ulinzi na Usalama na Kamati za Mazingira katika ngazi ya Mkoa, Wilaya, Tarafa, Kata, Vijiji na Mtaa.

“Kamati hizi zitawajibika kuwasilisha taarifa za operesheni wakati na baada ya operesheni hiyo Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na nakala Ofisi ya Makamu wa Rais,” ilisema taarifa hiyo na kuzitaja wizara na taasisi zinazohusika katika kamati hizo kuwa ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA); Mkemia Mkuu wa Serikali; Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS); Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Watoto na Wazee kupitia Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na mabwana afya; Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kupitia Idara ya Habari Maelezo itakayosaidia kutoa elimu kwa umma; Wizara ya Mambo ya Ndani, kupitia Jeshi la Polisi, na vyombo vingine vya ulinzi na usalama na pia Ofisi ya Makamu wa Rais na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira watakaoratibu operesheni.

Awali, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ndiye aliyeanza kutangaza amri ya serikali ya kupiga marufuku matumizi ya pombe kali za viroba kuanzia leo wakati akizungumza katika ziara yake mkoani Manyara aliyoifanya Februari 16, mwaka huu.

JESHI LA POLISI

Akizungumzia udhibiti wa pombe za viroba kuanzia leo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema kuwa tayari agizo limeshatolewa na Serikali na sasa kinachofuata ni utekelezaji tu, hivyo atakayebainika ana pombe za viroba atachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria za nchi.

“Katazo tayari limetolewa…watu wanatakiwa kutii sheria bila shuruti na wasiotii sheria watachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kuwakamata,” alisema Kamanda Mkumbo na kuongeza:

“Tayari kila mmoja ametangaziwa. Wananchi wanatakiwa kutii sheria na walipewa muda wa kutosha kujiandaa ili hivyo viroba visitumike tena, bali watengeneze chupa kubwa… asiyetaka kufuata agizo hilo tutamkamata.”

Aidha, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari, alisema suala hilo lipo kisera zaidi na hivyo wanasubiri mwongozo ili waingie mtaani mara moja.

Source: Nipashe
Viroba sasa vyageuka magendo kama bangi na 'unga' Viroba sasa vyageuka magendo kama bangi na 'unga' Reviewed by Zero Degree on 3/01/2017 10:11:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.