Loading...

Vita kati ya RC Makonda na Askofu Gwajima yaanza upya

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Josephat Gwajima, wameingia kwenye 'vita' mpya baada ya jana Askofu huyo wa Kanisa la Ufufuo na Uzima kulizungumzia tena sakata la madai ya mteule huyo wa Rais kutumia vyeti vya kitaaluma visivyo vyake ambalo alitangaza kulifunga wiki iliyopita.

Askofu Gwajima amekuwa akidai kuwa Makonda alitumia vyeti vya elimu ya sekondari vya Paul Christian Muyenge kupata elimu ya juu, huku akisisitiza kuwa jina halisi na Mkuu wa Mkoa huyo ni Daudi Albert Bashite.

Katika mahubiri yake ya jana kanisani kwake Ubungo jijini Dar es Salaam, Askofu huyo aliliibua tena sakata hilo, safari hii akisambaza kwa waumini wake nakala ya matokeo ya kidato cha nne ya kiongozi huyo wa serikali.

Askofu Gwajima alikwenda mbali zaidi kwa kuwataka waumini wake wakasambaze nakala hizo kwa kadiri wanavyoweza.

Wakati akisambaza nakala hizo, Askofu Gwajima alikuwa akisikika akisema: “Mwambie mwenzako, usiliamshe dude, utaumia".

Askofu huyo alisema alikuwa amepanga kutozungumzia tena suala hilo, lakini amelazimika kuendelea nalo kutokana na kile alichodai kuwa yeye ni mtu wa vita.

"Nilitaka kufunga mjadala ili kumsaidia (Makonda) ila kama mnavyojua, mimi ni mtu wa vita tangu ujana wangu. Nikisikia sauti ya risasi za vita, moyo unawaka na kurudi vitani, wanaosema 'amen' waseme ameeen," alisema huku waumini wake wakisema 'ameeeen'.

Katika mafundisho yake ya jana, Askofu Gwajima alikuwa na somo lenye kichwa cha habari 'Nitavunjavunja magari ya chuma'.

Tofauti na ilivyokuwa imezoeleka, ibada hiyo haikuonekana moja kwa moja kupitia U-Tube na Facebook, licha ya Askofu huyo kueleza awali kuwa ingeonekana kuanzia saa 4:00 asubuhi.

Kuonyeshwa kanisani kwa nakala ya matokeo ya mtihani wa kidato cha nne ya Daudi Albert Bashite, kumejitokeza ikiwa ni wiki moja baada ya Askofu Gwajima kuwaeleza waumini wake kuwa amefunga mjadala wa Bashite hadi pale atakapochokozwa tena.

Alisema kuwa maelezo yake kuhusu uhusiano wa Makonda na Bashite yataendelea kubaki vilevile huku akisisitiza kuwa sakata hilo kwake ni ‘past tense’ (lililopita).

KUTELEKEZA MTOTO

Askofu Gwajima pia alizungumzia tuhuma za yeye kutelekeza mtoto ambazo ziliibuka juzi na kuenea kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii zikiambatana na video na picha za mnato za mwanamke akiwa na mtoto mdogo akidai amezaa na mtumishi huyo wa Mungu.

Taarifa hizo pia ziliambatana na kadi ya kliniki ya mtoto aliyezaliwa Desemba 3, 2016, akiwa na kilo tatu. Kadi hiyo inaonyesha jina la mama wa mtoto na la anayedaiwa kuwa baba, Josephat Mathias Gwajima.

Kadi hiyo mbali na kutotaja jina la mtaa wala kijiji wanakoishi wazazi wa mtoto huyo, pia inaonyesha mtoto huyo alipata chanjo ya kwanza Desemba 16, mwaka jana, yaani siku 13 baada ya kuzaliwa na nyinginezo anatakiwa kupata Desemba 19 na 20, mwaka huu.

Askofu Gwajima, akizungumzia suala hilo kanisani kwake jana, alidai mwanamke anayeonekana kwenye video hiyo ni mgonjwa wa akili na kwamba anamfahamu mumewe (alitaja jina lake) na kusisitiza kuwa nyumbani kwao ni Ubungo jirani na kanisa hilo.

"Juzi nilikutana na baba mkwe wake na huyo mwanamke tukizungumza mambo kadha wa kadha, kesho (leo) watakuwepo kanisani watazungumza," alisema Askofu Gwajima.

"Jumatano iliyopita, Daudi Bashite alimchukua mwanamke kichaa, kanisa lote mnajua ni kichaa, mume wake na baba mkwe wake tutakuwa naye hapa."

Askofu Gwajima alisema alijipanga kumzungumzia mtangazaji wa kituo kimoja cha runinga, lakini amemweka kiporo ili aendelee na suala la Bashite.

Alifafanua kuwa walimchukua mwanamke huyo Jumatano usiku eneo la Sinza Mori, karibu na Wanyama Hotel wakarekodi na kumsumbua mama huyo aseme alikuwa ana uhusiano na Askofu Gwajima na amezaa naye.

Aliwaeleza waumini wake kuwa siyo ajabu kuzaa na kwamba wakiambiwa mchungaji wao kazaa mahali fulani, wasishangae kwa kuwa anaongeza idadi ya waumini.

Alidai video ya mwanamke huyo ilisambazwa baada ya kuchukuliwa kwa nguvu kutoka kwa mtangazaji mmoja (jina tunalihifadhi) na kuisambaza kwenye mitandao ya kijamii.

Akifafanua kuhusu matokeo ya mtihani wa kidato cha nne anayodai kuwa ya Makonda, Askofu huyo alisema kwa kawaida mtu akipata daraja sifuri, hapewi cheti lakini kwenye tovuti ya Baraza la Mitihani (Necta), yanaonekana.

"Nimetoa 'copy' (nakala) kadha wa kadha, nitawapa kila mtu mgawiane huko njiani, kila mtu agawanye," alisema Askofu Gwajima huku waumini wakishangilia na kupokea nakala hizo za matokeo ya kidato cha nne ya Bashite.

Askofu Gwajima alisoma moja ya nakala hizo mbele ya waumini wake na kueleza matokeo ya kila somo kuwa alipata alama F kila somo likiwamo huku akifuatiliwa na waumini wake kutaja na kuwalipua kwa shangwe zaidi alipoeleza kuwa hata somo la Biblia mpinzani wake huyo alipata alama F.

“Yaani, wiki hii nzima nitakuwa kazini. Apigweeeee!" Waumini wakaitikia 'apigweeee!'

"Sasa mjiulize mtu amepata sifuri hadi Biblia, Kiswahili na Kiingereza, kwa maneno mengine kamaliza darasa la saba halafu anachukua vyeti vya mtu. Ameachiwa Dar es Salaam aiharibu na hakuna wa kumkemea.

"Naomba watu wote tusichukuliwe na jambo lolote tusisitize vyeti, vyeti," aliongeza Askofu Gwajima huku kanisani kukisika sauti za waumini wake wakisema "vyeti, vyeti, vyeti..."

Nakala ya matokeo hayo iliyoonyeshwa jana na Askofu Gwajima, inaonyesha matokeo hayo ni ya mwaka 2000, na mhusika alifanya mtihani kwa usajili wa namba ya shule S0546 Pamba Sekondari, namba ya usajili ya mwanafunzi ni S0546/0016 na jina lake Daudi A. Bashite, akiwa amepata daraja sifuri na pointi 35.

Kwa takribani miezi mwili sasa, suala la uhalali wa vyeti vya kitaaluma vya Makonda limezua mjadala ambao umenogeshwa zaidi Askofu Gwajima anayedai alitumia cheti cha mtu kujiunga na elimu ya juu na majina anayotumia siyo yake kwa kuwa anamfahamu kwa jina Daudi Albert Bashite.

Askofu Gwajima amedai zaidi kuwa yeye na Makonda wanatoka eneo moja wilayani Misungwi mkoani Mwanza na baba yake ni miongoni mwa askari waliokuwa kwenye Vita vya Kagera (1979-1980).

Askofu Gwajima, katika kutetea hoja yake, amekuwa akisisitiza kuwa Makonda alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Koromije wilayani Misungwi ambako yeye na baba yake wanatoka huku akitaja majina na ndugu zake waliosoma na Mkuu wa Mkoa huyo.

Hadi sasa, Makonda hajajitokeza hadharani kukanusha au kufafanua juu ya uhalali wa vyeti vyake vya masomo ya shule ya msingi, sekondari na chuo kikuu.

Kabla ya tuhuma za udanganyifu wa elimu, Makonda alikuwa amemtaja Askofu Gwajima katika orodha ya watu 65 waliotakiwa kuisaidia polisi kuhusu biashara ya mihadarati.

Askofu Gwajima ambaye amekanusha hadharani kuhusika kwa namna yoyote na dawa za kulevya, alipimwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali na kugundulika kuwa si mtumiaji.

Kabla ya kutaja orodha hiyo iliyokuwa pamoja na Gwajima, wafanyabiashara na wanasiasa, Makonda alikuwa ametoa orodha ya Polisi 12 na wasanii kadhaa ambao walitakiwa pia kufika Kituo Kikuu cha Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa mahojiano.

Source: Nipashe
Vita kati ya RC Makonda na Askofu Gwajima yaanza upya Vita kati ya RC Makonda na Askofu Gwajima yaanza upya Reviewed by Zero Degree on 3/20/2017 10:40:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.