Loading...

Jinsi ajali za Bodaboda zilivyopungua baada ya viroba kupigwa marufuku

Ajali ya bodaboda (Picha ya mtandao).
TAASISI ya Mifupa Muhimbili (MOI), imesema idadi ya majeruhi watokanao na ajali za bodaboda imepungua kutoka 25 hadi watano kwa siku, jambo ambalo limesaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa.

Kutokana na kupungua huko, Kadhalika, MOI imesema itafanya utafiti wa kubaini kama kupungua kwa ajali hizo imesababishwa na kupigwa marufuku kwa uuzwaji wa pombe kali zilizofungashwa kwenye mifuko ya plastiki, maarufu kama viroba, kutokana na baadhi ya majeruhi kufikishwa hospitalini hapo wakiwa na harufu ya pombe.

Msemaji wa taasisi hiyo, Jumaa Almasi, alisema hayo juzi alipohojiwa na Nipashe kuhusiana na kupungua kwa ajali hizo. Alisema kwa kiwango kikubwa ajali zimepungua ikilinganishwa na mwaka jana.

Alisema kwa sasa wanapokea wagonjwa watano hadi saba kwa siku wakati mwaka jana katika kipindi cha Machi, mwaka jana, walipokea majeruhi 190 na kwa mwaka huu kipindi kama hicho, walipokea wagonjwa 81.

Almasi alisema kupungua kwa ajali hizo kumechangiwa na elimu inayotolewa na askari wa usalama barabarani kwa kuwa vijana kwa sasa wana uelewa mkubwa ikilinganishwa na awali.

Alisema majeraha ya kichwani yamepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na wengi wao kuvaa kofia ngumu kichwani pamoja na kufuata sheria za barabarani.

TAKWIMU ZA AWALI


Takwimu za MOI za majeruhi hao zinaonyesha kuwa Februari, mwaka jana, idadi ya majeruhi ilikuwa 223 wakati Februari mwaka huu ilikuwa 117 na Januari, mwaka jana, walikuwa 269 na wakati kipindi kama hicho kwa mwaka huu walikuwa 137.

Almasi alisema kumekuwa na mabadiliko ya idadi ya majeruhi wanaopokewa MOI, ikiwamo aina ya majeraha wanayopata.

Alisema kwa sasa majeruhi waliokuwa wakiumia zaidi maeneo ya kichwa wamepungua, ikilinganishwa na maeneo mengine ya mwili.

Alisema majeruhi hao wanaopokewa zaidi ni wale walioumia maeneo ya miguu, mikono na maeneo mengine ya mwili ni si kichwani.

“Kuna sababu nyingi ambazo kwa uchunguzi wa awali inaonyesha elimu ya usalama barabarani kutoka kikosi cha usalama barabarani imeongezeka. Mara nyingi wanashirikiana na sisi (MOI), tumebaini kuwa elimu ya uvaaji kofia ngumu (helmet) imeongezeka,” alisema Almasi.

Alisema sababu nyingine ni mpango wa askari wa usalama barabarani kufanya maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama kila mwaka, kwenye vituo vikubwa vya usafiri ikiwamo vya daladala na hata mabasi yaendayo mikoani.

Alisema wakati taasisi hiyo ikiwa kwenye hatua za kufanya utafiti ili kubaini sababu rasmi ya kupungua kwa majeruhi wa ajali hizo, sababu nyingine ya kupungua inaweza kuwa madereva wa bodaboda kuacha kunywa wakiwa kazini.

“Mara nyingi majeruhi ambao walikuwa wanaletwa hapa, wengi walikuwa wakikutwa na harufu ya pombe na baadhi wamelewa kabisa. Hata hivyo, hatujabaini kama ni pombe ya aina gani, lakini kiujumla bado utafiti unahitajika,” alisema Almasi.

Alisema nchi kwa sasa inaelekea kufanikiwa katika kupunguza idadi ya ajali, hususan bodaboda kwa kukazia elimu zaidi kutolewa kuhusu uvaaji wa kofia ngumu, kwa abiria na dereva ikizingatia kwamba usafiri huo umekuwa ni maarufu kwa maeneo ya mjini na vijijini.
Jinsi ajali za Bodaboda zilivyopungua baada ya viroba kupigwa marufuku Jinsi ajali za Bodaboda zilivyopungua baada ya viroba kupigwa marufuku Reviewed by Zero Degree on 4/08/2017 12:05:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.