Loading...

Jinsi mkopo wa milioni 400 ulivyowaponza maaskofu

Askofu Mkuu wa AICT Tanzania, Askofu Silasi Kezakubi
MAASKOFU wa Kanisa la African Inland Church of Tanzania (AICT), Dk John Nkola wa mkoani Shinyanga na mwenzake wa Dayosisi ya Mwanza, John Bunango wametakiwa wajiuzulu nafasi hiyo kwa kushindwa kusimamia vizuri fedha za mkopo Sh milioni 400 walizokopa Benki ya CRDB kuendesha miradi mbalimbali.

Aidha, wengine waliowajibishwa kwa kuvuliwa madaraka ya uchungaji ni Emmanuel Isaya, Dk Meshack Kulwa na Jakobo Mapambano aliyekuwa Katibu Mkuu wa kanisa hilo Dayosisi ya Shinyanga.

Askofu Mkuu wa AICT Tanzania, Askofu Silasi Kezakubi alisema hayo mbele ya waumini wa kanisa hilo mjini Shinyanga lililopo Kambarage wakati wa ibada ya Jumapili jana huku akieleza kuwa maamuzi ya kuwachukulia hatua viongozi hao yametokana na kikao cha Baraza la Utendaji la Sinodi Kuu AICT.

Askofu Kezakubi alisema viongozi hao wamelitia aibu kanisa kwa kushindwa kusimamia vizuri fedha kiasi cha Sh milioni 400 zilizokopwa katika Benki ya CRDB mwaka 2008 kwa ajili ya kuendesha Shule ya Sekondari Bishop Nkola na kusababisha kupigwa mnada kwa kutorejesha deni.

Alisema taarifa za mradi huo zilikuwa hazitolewi, kwani ilikuwa siri ya watu wachache, na kufikia kushitukizwa shule kuuzwa bila ya wao kujua na kuridhia ipigwe mnada.

Aliongeza kuwa ilibainika kuwa kuuzwa kwa shule hiyo kunatokana na kwamba kulikuwa na matumizi mabaya ya fedha za mkopo kutoka benki na fedha za harambee mbili zilizofanyika kanisani hapo na tatizo la kutotoa taarifa kwenye vikao vya ngazi za juu, kwani ngazi za juu zilishtukizwa tu kuwa shule imeuzwa.

“Kwa sababu ya mzigo wa uongozi na yeye kama msimamizi Baraza la Utendaji liliamua kumuomba Askofu Nkola astaafu sasa na alipopokea barua hakuwa na maneno ya kukataa na sisi tunampongeza kuchukua moyo huo kwa kuwajibika,” alieleza Askofu Mkuu Kezakubi.

Alisema kosa la Askofu Nkola ni kushindwa kusimamia watendaji wake vizuri ili jambo hilo lisitokee vile alikuwa hajatoa taarifa kwenye mabaraza ya juu kuhusu jambo hilo.

Pia baraza limechukua hatua pia kwa watendaji waliokuwa katika Ofisi ya Askofu Nkola, kwa kumuomba aliyekuwa Katibu Mkuu wa AICT Dayosisi ya Shinyanga, John Bunangwa ambaye sasa ni Askofu wa Kanisa la AICT, Dayosisi ya Mwanza naye ajiuzulu nafasi yake ya uaskofu.

Alisema Askofu Bunangwa anachukuliwa hatua kwa kutosimamia vizuri fedha za kanisa Sh milioni 400 za mkopo kutoka CRDB na za harambee iliyoendeshwa kanisani hapo na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye zilipatikana Sh milioni 200 ambazo kama kungekuwa na uwazi, zingepunguza deni hata kidogo.

Askofu huyo aliongeza kuwa Bunangwa pia alishindwa kusimamia urejeshaji wa mkopo huo kwa sababu hata akiwepo, kulikuwa na matatizo na kushindwa kutumia wataalamu katika kuvunja baadhi ya mikataba aliyokuwa anaisimamia na kusababisha hasara kubwa katika kanisa.

Aidha, Bunangwa aliruhusu ongezeko kwenye mikataba mbalimbali bila kufuata utaratibu wa kuongeza gharama za miradi hiyo.

Kezakubi alisema baraza pia limemvua uchungaji Katibu Mkuu wa AICT Dayosisi ya Shinyanga, Mapambano kwa kushindwa kupeleka taarifa sahihi katika vikao vya juu tangu kuanza kwa tatizo la shule.

Alisema pia baraza hilo limemuondoa uchungaji Emmanuel Isaya aliyekuwa kwenye Kitengo cha Elimu, ambaye aliidhinisha malipo kinyume cha mamlaka yake na kushindwa kusimamia ujenzi wa majengo ya shule.

Pia limemwondolea uchungaji Dk Meshack Kulwa kwa makosa ya kimaadili.

Akijibu tuhuma hizo, Askofu Nkola alisema amewajibishwa kutokana na makosa yaliyofanywa na watendaji wake wa chini, kwani hata tume iliyoundwa kuchunguza haikuona kama amehusika na ubadhirifu wa fedha.

Alisema kutokana na kanuni, sheria na taratibu zake kama kiongozi aliyeongoza waumini na kanisa, amepokea maamuzi yaliyochukuliwa kwa moyo mweupe kabisa, na atastaafu Mei 25, mwaka huu baada ya kulitumikia kanisa tangu mwaka 1993.

Mchungaji Mapambano alikiri kutenda makosa yaliyotajwa na kuongeza kuwa matatizo katika shule hiyo aliyarithi mwaka 2010 kutoka kwa aliyekuwa katibu wa kanisa hilo Bunangwa ambaye sasa ni askofu wa kanisa hilo Dayosisi ya Mwanza aliyeombwa kujiuzulu nafasi hiyo.
Jinsi mkopo wa milioni 400 ulivyowaponza maaskofu Jinsi mkopo wa milioni 400 ulivyowaponza maaskofu Reviewed by Zero Degree on 4/03/2017 12:04:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.