Loading...

Maalim Seif sasa amgeukia Msajili wa Vyama vya Siasa

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff ameituhumu Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania kuwa, inashinikiza Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) ipitishe majina ya wajumbe wa bodi ya wadhamini yaliyopelekwa na upande wa Profesa Ibrahim Lipumba.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Maalim Seif alisema Rita wakipitisha majina yaliyopelekwa na upande wa Lipumba wawe tayari kubeba dhamana kwa yatakayotokea.

“Tunajua Msajili amekuwa akiwasiliana na Rita kutia shinikizo wajumbe feki wa bodi ya udhamini ndiyo wasajiliwe,” alisema.

Alisema kikao cha Baraza la Uongozi la Taifa la CUF kilichofanyika Zanzibar Machi 19, kilipitisha majina ya wajumbe wa bodi ya wadhamini ili kufanya mabadiliko madogo na kuyapeleka Rita.

Maalim Seif alisema baada ya kupeleka majina hayo, wamepata taarifa zisizo na shaka kwamba upande wa Profesa Lipumba nao umepeleka majina yao Rita.

“Tumevumilia kiasi cha kutosha sasa basi nawahakikishia kwamba tutailinda CUF kwa gharama yoyote ile na mlio nyuma ya hujuma hizi mtabeba dhamana kwa yatakayotokea,” alisema.

Akizungumzia hilo, Kaimu Ofisa Mtendaji wa Rita, Emmy Hudson alisema yeye atafuata sheria na kwamba hadi sasa hajapata shinikizo kutoka sehemu yeyote.
Maalim Seif sasa amgeukia Msajili wa Vyama vya Siasa Maalim Seif sasa amgeukia Msajili wa Vyama vya Siasa Reviewed by Zero Degree on 4/10/2017 12:03:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.