Loading...

Mauzo ya hisa katika Soko la Hisa Dar [DSE] yapanda zaidi ya mara tatu

Idadi ya hisa zilizouzwa na kununuliwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) imeongezeka zaidi ya mara tatu kutoka hisa 520,000 hadi hisa 1,700,000 zenye thamani ya mauzo ya Sh. Bilioni 13.9 kutoka Bilioni 1.8 wiki iliyoishia Aprili 7,2017.

Afisa Masoko na Mauzo DSE, Patrick Mususa wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, amesema Mtaji wa kampuni za ndani umeendelea kubaki kwenye kiwango cha awali cha Sh. Trilioni 7.507.

Hata hivyo, amesema kufuatia kupungua kwa bei za hisa za JUBILEE HOLDINGS kwa asilimia 7.7 na ACACIA 4%, Ukubwa wa mtaji wa kampuni zilizoorodheshwa katika soko umepungua kutoka Sh. Trilioni 20.1 hadi kufikia Sh. Trilioni 20.

Hali kadhalika amesema kiashiria cha kampuni zilizoorodheshwa katika soko kimeshuka kwa pointi 18 kutoka pointi 2,315 hadi pointi 2,297 kutokana na kupungua kwa bei za hisa za kampuni mbali mbali zilizopo sokoni, wakati Kiashiria cha kampuni za ndani kikiendelea kubaki kwenye wastani wa pointi 3,573 wiki hadi wiki huku Sekta ya viwanda ikiendelea kubaki kwenye kiwango cha awali cha pointi 4,618.

“Sekta ya huduma za kibenki na kifedha (BI) wiki hii i imeendelea kubaki kwenye kiwango cha awali cha pointi 2,546.Sekta ya huduma za kibiashara (CS) wiki hii imebaki kwenye kiwango cha awali cha pointi 3,137,” amesema.

Katika hatua nyingine, amesema mauzo ya hati fungani yameshuka kutoka thamani ya Sh. Bilioni 22.4 wiki iliyopita hadi Bilioni 12.1 kutokana na mauzo ya hati fungani 6 za serikali na hati fungani 1 ya NMB Bank zenye jumla ya thamani ya Bilioni 17.2 kwa jumla ya gharama ya Shilingi Bilioni 12.1.

Pia ametaja shule na vyuo vilivyoongoza kuwa na idadi kubwa ya washiriki katika Shindano la Wanafunzi la Uwekezaji, ikiwemo chuo cha Uhasibu Arusha IAA, Chuo cha Mipango(IRDP) na shule ya sekondari Loyola.
Mauzo ya hisa katika Soko la Hisa Dar [DSE] yapanda zaidi ya mara tatu Mauzo ya hisa katika Soko la Hisa Dar [DSE] yapanda zaidi ya mara tatu Reviewed by Zero Degree on 4/10/2017 11:50:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.