Loading...

Raia watatu wa kigeni wamekamatwa na Pembe za Ndovu jijini Dar

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishina Simon Sirro
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia raia wawili wa nchi ya Afrika Kusini na mmoja wa Serbia baada ya kuwakamata na pembe mbili za ndovu zinaokadiriwa kuwa na uzito wa kg 45.

Wakati akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishina Simon Sirro amesema awali walipokea taarifa kutoka kwa rai wema kwamba kuna wafanyabiashara watatu wanashukiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na kwamba baada ya polisi kufanya ukaguzi hawakuwakuta na dawa hizo badala yake walipatikana na pembe mbili za ndovu.

“Mnamo tarehe Machi 28, 2017 maeneo ya Upanga mtaa wa Charambe polisi wafanya ufuatiliaji wa taarifa za wafanyabiashara watatu wa kigeni wanaoshukiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya zilizotolewa na raia wema, walipopekuliwa hawakupatikana na dawa hizo badala yake walipatikana na pembe mbili za ndovu,” amesema.

Amesema upelelezi kuhusu shauri hilo unaendelea kwa kufanya mawasiliano na idara ya maliasili ili kubaini kama watuhumiwa wanamiliki nyara hizo za serikali kihalali.

Katika hatua nyingine, Kamanda Sirro amesema Jeshi la Polisi kuanzia Machi 29 hadi Aprili 5, 2017 limekamata watuhumiwa 40 wa dawa za kulevya pamoja na 306 wanaotuhumiwa kwa makossa mbalimbali ya kihalifu ikiwemo wizi wa vifaa vya magari, unyang’anyi wa kutumia nguvu na mauaji.

Aidha, amewatahadharisha wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kuhusu matapeli wanaotumia majina ya kampuni kuwatapeli watu fedha kwa minajili ya kuwatafutia kazi. Pia ametoa tahadhari kuhusu mvua zinazoendelea kunyesha na kuwataka watu kuacha kuzibua vyoo vyao na kuyaelekeza maji machafu barabarani na kwenye makazi ya watu.

“Kipindi hiki cha mvua kumekuwa na tabia kwa baadhi ya watu kuacha wazi mashimo waliyochimba kwa ajili ya vyoo, takataka na au karo jambo ambalo maji yakijaa hayaonyeshi kina chake ambapo mtu akipita juu yake huweza kuzama na kupoteza maisha au kupata madhara mengine,” amesema.

Hata hivyo, Kamanda Sirro amesema Kikosi cha Usalama Barabarani cha Kanda hiyo kuanzia Machi 29 hadi Aprili 4, 2017 kimetoza faini ya 612,060000 kutokana na makosa ya barabarani 20,385.

Source: DewjiBlog
Raia watatu wa kigeni wamekamatwa na Pembe za Ndovu jijini Dar Raia watatu wa kigeni wamekamatwa na Pembe za Ndovu jijini Dar Reviewed by Zero Degree on 4/06/2017 01:05:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.