Loading...

Serengeti Boys yaonja joto la Mamlaka ya Mapato Tanzania [TRA]

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) jana ilishusha msafara wa timu ya taifa ya chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys na kukamata basi walilokuwa wakilitumia.

Serengeti ilikutana na zahama hiyo ikiwa nje ya kambi yao maeneo ya Kisutu Dar es Salaam tayari kwa safari ya kwenda kupata chakula cha jioni na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ambaye aliwaalika kuwaaga.

Timu hiyo inayotarajiwa kushiriki fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa vijana mjini Gabon mwezi ujao, inatarajiwa kuondoka leo mchana kwenda Morocco kwa kambi ya maandalizi.


Akithibitisha taarifa hizo, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas alisema basi hilo ambalo hutumiwa na timu ya soka ya taifa ya wakubwa, Taifa Stars lilikamatwa na kampuni ya udalali na minada ya Yono.

Takriban wiki tatu sasa, TRA imefunga ofisi na kuzuia baadhi ya mali za TFF kutokana na deni kubwa la malimbikizo ya kodi za mishahara ya aliyekuwa kocha wa Taifa Stars, Mbrazili Marcio Maximo kwa miaka minne tangu mwaka 2006- 2010.

Deni lingine linalosababisha ofisi za TFF kufungwa ni la Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) la ziara ya timu ya taifa ya Brazil nchini mwaka 2010 ilipokuwa njiani kwenye Afrika Kusini kwenye fainali za Kombe la Dunia.

TRA laliachia basi la Serengeti Boys:

Mamlaka ya mapato nchini, TRA imeliachia basi la shirikisho la soka nchini, TFF lililokuwa limekamatwa na wakala wake wa udalali, Yono kutokana na limbikizo la madeni. Kampuni ya Yono ililishikilia kwa muda basi hilo jana.

Taarifa ya TFF kupitia mitandao ya kijamii imesema: Nathibitisha kuwa Kampuni ya Udalali ya Yono ambayo ni Wakala wa TRA imetangaza kuliachia gari mara moja basi linalotumiwa na wachezaji wa Serengeti Boys na wameomba nilifuate hata sasa, usiku huu. Wamefuata amri ya TRA. Tutalifuata asubuhi, ili liendelee na shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwapeleka vijana wetu Airport kuwahi ndege kwani vijana wetu wanatarajia kuondoka jioni.

Naye Rais wa TFF, Jamal Malinzi ameandika hivi kwenye ukurasa wake wa tweeter: Basi la TFF limeachiwa usiku huu.Suala hili la kodi tukijaliwa tutalimaliza vizuri tu kwa majadiliano.Usikimbilie kuhukumu.”

Awali wao wenyewe TRA waliandika: TRA inasikitishwa na kitendo cha mmoja wa mawakala wa kudai madeni kwa kukamata gari la Serengeti Boys bila kujali wala kuzingatia utaratibu. Imethibitisha agizo la kuachiwa kwa gari hiyo limetekelezwa, wakati taratibu zingine za kiutendaji zikiwa zinaendelea kwa wahusika.
Serengeti Boys yaonja joto la Mamlaka ya Mapato Tanzania [TRA] Serengeti Boys yaonja joto la Mamlaka ya Mapato Tanzania [TRA] Reviewed by Zero Degree on 4/05/2017 01:05:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.