Loading...

Serikali za mitaa kupewa ruhusa ya kutoa PF3?

SERIKALI imesema itaangalia uwezekano wa kuanzisha utaratibu wa viongozi wa serikali za mitaa kutumiwa kutoa fomu za polisi kwa ajili ya matibabu (PF3) panapotokea majeruhi, badala ya kutegemea Jeshi la Polisi pekee.

Hayo yamesemwa bungeni mjini Dodoma na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Mwanne Mchemba (CCM) aliyetaka kufahamu kama utolewaji wa fomu hizo unaweza kurahisishwa.

Mbunge huyo amesema watu wengi na hasa wanawake wamekuwa wakiogopa kwenda vituo vya polisi zinapotolewa fomu hizo za PF 3 na hivyo kusababisha majeruhi kuteseka na wengine kupoteza maisha.

Amesema, serikali inapaswa kutoa kama itaweza kurahisisha mlolongo wa utoaji wa fomu hizo ili ikiwezekana zianze kutolewa katika ngazi za wenyeviti wa vijiji, mitaa na vitongoji.

Mwigulu akijibu alisema ushauri uliotolewa na mbunge huyo ni mzuri na hivyo serikali itawasiliana na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ili kuangalia namna mpango huo unavyoweza kufanyiwa kazi.

Amesema uamuzi wa kuruhusu fomu za PF3 kutolewa katika ngazi za wenyeviti wa mitaa, vijiji na vitongoji umekuwa unakwama kutokana na ukweli kuwa utaratibu wa kutolewa polisi hutumika pia katika kuwanasa watu wanaojeruhiwa wakiwa katika matukio ya uhalifu wakiwemo majambazi.

"Pale inapotokea watu wamejeruhiwa halafu hawajafika polisi kuchukua PF 3 tunajua fika kuwa ni wahalifu na tunajua namna nzuri ya kuweza kuwanasa.

Hata hivyo, ushauri huu wa mbunge wa kuangalia jinsi wenyeviti wa vijiji, mitaa na vitongoji wanavyoweza kutumiwa katika kurahisisha utolewaji wa PF3 tutaufanyia kazi, hasa kwa wale wanaopata majeraha wakiwa katika ngazi za familia ambao wanafahamika kuwa hawana rekodi za uhalifu basi wapatiwe fomu hizo," ameongeza.

Akijibu swali la msingi, waziri huyo alisema serikali iliweka utaratibu wa mtu anapokuwa ameumia apate PF3 kwa mujibu wa kifungu cha 170 cha Kanuni za Kudumu za Jeshi la Polisi (PGO) ili aweze kupokewa na kupewa matibabu katika hospitali.

Amesema msingi mkubwa wa fomu hiyo ni kutaka kujua mazingira ya mtu huyo aliumia wapi na alikuwa anafanya nini.

Alisema PF 3 inatumika pia kama kielelezo mahakamani kama mtu ameshambuliwa ama amepigwa ili mahakama ijue ameumia kiasi gani na kuwa rahisi kutoa adhabu stahiki.

Amesema hata hivyo kuna matukio mengine yaliyo wazi PF 3 hupelekwa hospitali kwa urahisi wa matibabu na kwa msingi huo fomu hiyo bado inakidhi matakwa yaliyokusudiwa.
Serikali za mitaa kupewa ruhusa ya kutoa PF3? Serikali za mitaa kupewa ruhusa ya kutoa PF3? Reviewed by Zero Degree on 4/11/2017 11:49:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.