Loading...

TANZIA: Mwandishi wa habari, Josephat Isango amefariki dunia leo asubuhi akiwa hospitali

Tasnia ya Habari nchini imepata pigo kubwa baada ya kuondokewa na Mwandishi wa Habari Bwana Josephat Isango ambaye amefariki Dunia asubuhi ya leo majira ya saa moja na na dakika 10, wakati akiwa amelazwa Hospitali ya Mt. Maria, Malkia wa Ulimwengu Puma iliyopo Wilaya ya Ikungi, Mkoani Singida.

Mdogo wa Marehemu amethibitisha na kueleza kuwa kwa sasa msiba upo kijijini kwao Kisasidi huku mwili wa marehemu ukiwa umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Singida.

“Ni kweli Josephat Isango amefariki asubuhi ya leo majira ya saa moja. Alikuwa hapa anapatiwa matibabu akiwa anasumbuliwa na matatizo ya moyo. Taratibu zingine zinaendelea nyumbani huko Kijijini KIsasidi” alieleza Mdogo huyo wa Marehemu.

Hata hivyo alieleza kuwa, wamepanga kufanya maziko siku ya Aprili 18 ambayo itakuwa Jumanne majira ya saa nne asubuhi huko huko Kijijini kwao Kisasida, Barabara ya Arusha.

Marehemu Isango ni miongoni mwa wanahabari mahili na mwenye weledi mkubwa katika tasnia ya Habari huku akiwa amepitia vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini. Miongoni mwa vyombo alivyofanyia kazi ni pamoja na kampuni ya Free Media Limited wachapishao magazeti ya Tanzania Daima, Pia aliwahi kuwa mwandishi wa habari wa kampuni ya Halihalisi Publishers inayochapisha magazeti ya Mwanahalisi, Mawio na Mwanahalisi On line na baadae alikuwa Jamii Media.

Marehemu Isango amefariki akiwa na umri wa miaka 44, huku akiwa ni mtoto wa 5 wa familia ya Mzee Isango.

Marehemu mbali na kuwa na taaluma ya Habari, pia mwaka 2010 aliwahi kuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Singida mjini kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) huku akichuana vikali na mgombea mwenzake wa wakati huo alikuwa Mohammed Dewji ‘MO’’.


Mtandao huu wa Zero Degree, unatoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki pamoja na wanatasnia ya habari popote pale walipo, Ameni.

Source: DewjiBlog
TANZIA: Mwandishi wa habari, Josephat Isango amefariki dunia leo asubuhi akiwa hospitali TANZIA: Mwandishi wa habari, Josephat Isango amefariki dunia leo asubuhi akiwa hospitali Reviewed by Zero Degree on 4/14/2017 04:58:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.