Loading...

Viongozi wa Taasisi za kidini nchini wahimizwa kueneza amani na upendo

Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu kwa jamii ya madhehebu ya dini zote nchini, Askofu William Mwamalanga amezihimiza taasisi za Dini nchini kueneza masuala ya amani na upendo ili kuendelea kuilinda amani tuliyonayo kwa muda mrefu sasa.

Askofu Mwamalanga amesema hayo jana Aprili 5.2017 wakati wa kutoa pongezi na kumteua Sheikh Harith Nkussa kuwa Mjumbe wa Kamati ya amani Kitaifa baada ya kuonekana kueneza vyema masuala ya amani hapa nchini.

Akisoma taarifa juu ya uteuzi huo, Askofu Mwamalaanga amebainishakuwa, Kamati yao imebaini kuwa Sheikh Nkussa amekuwa ni miongoni mwa Masheikh wanaofanikisha amani hapa nchini kwani kwa hatua yake ya kutembelea katika kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima lililopo Ubungo Jijini Dar es Salaam ni kielelezo tosha cha amani kwani viongozi wa dini kwa pamoja wanahubiri amani na upendo.

“Sote tuliona na tumeona. Sheikh Nkussa kwenda kwake kanisani hakusema yeye katumwa na nani wala taasisi iliyomtuma bali alielezea suala la amani ya nchi yetu. Kamati tumeona huyu ni mmoja wa watanzania wenye ucbungu wa nchi hii na tunamteua kuwa mjumbe wa kamati zetu.” Alieleza Askofu Mwamalanga.

Ameongeza kuwa, mataifa karibu yote yanaitamani Amani ya Tanzania hivyo suala la viongozi wa dini kuwa na hali ya kutembeleana ni ishara tosha kuwa ukubwa wa amani yetu ni ya kuungwa mkono na pande zote huku akiwataka viongozi wa dini kuachana na tabia ya kubeza hali hiyo.

“Kamati ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu na mimi nikiwa Mwenyekiti wake. Uchunguzi tuliofanya umebainisha kuwa, Sheikh Nkussa alifanya jambo jema sana kutembelea kanisani. Jambo lile ni la kuungwa mkono na kila mmoja wetu kwani pia ameonyesha nia njema na ya dhati katika kuunganisha pande zote mbili na ametekeleza wajibu wake”ameeleza Askofu Mwamalanga.

Aidha, Askofu Mwamalanga ameeleza kuwa, kupitia Kamati ya Amani, ametoa wito kwa Serikali ya Tanzania, taasisi za Kikristo, taasisi za Kiisla na Mabaraza yake kuendelea kumtumia Sheikh Nkussa katika juhudi za kuendeleza umoja na utangamano mwema baina ya watanzania.

Kwa upande wake, Sheikh Nkussa ameishukuru Kamati hiyo kwa kuona umuhimu wake ambapo amesema kuwa, yeye atabaki kuwa Sheikh wa Kata anayetambulika na taasisi husika ya dini hiyo ya Kiislam hapa nchini huku akieleza kuwa, usomi wake katika elimu ya dini ya kiislam ndio nguzo kuu anayoiamini yeye na wala si nyingine.

Kamati ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu kwa jamii ya madhehebu ya dini zote nchini,inayoongozwa na Askofu William Mwamalanga awali ilibainisha kuwa, tukio la Sheikh huyo kutembelea katika kanisa la Ufufuo na Uzima lilizua hisia tofauti kwa upande wa moja ya taasisi za dini ya Kiislam na kupelekea kutoa tamko kuwa hawakuhusika kumtuma kufanya hivyo.
Viongozi wa Taasisi za kidini nchini wahimizwa kueneza amani na upendo Viongozi wa Taasisi za kidini  nchini wahimizwa kueneza amani na upendo Reviewed by Zero Degree on 4/07/2017 04:53:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.