Loading...

Wafugaji wakorofi wakamatwe na kuchukuliwa hatua, Waziri mkuu

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Injinia Evarist Ndikilo apige kambi katika kata ya Miono wilayani Bagamoyo na kuwasaka wafugaji wanaopiga wakulima.

Alitoa agizo hilo wakati akizungumza na wakazi wa kata hiyo ambao walisimamisha msafara wake wakati akienda kukagua miundombinu ya Hifadhi ya Taifa ya Saadani iliyoko wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani.

Akitoa kero za eneo hilo, Diwani wa Kata ya Miono, Juma Mpwimbwi alisema kata hiyo inakabiliwa na tatizo la wakulima kupigwa na wafugaji na wakipelekwa kituo cha polisi hawachukuliwi hatua yoyote.

“Wafugaji wanatupiga lakini wenzetu hawachukuliwi hatua na hata ukienda kushtaki polisi, hawakai kwa sababu wanadai wao wana fedha,” alisema diwani huyo.

Alisema pia mbali ya kero sugu ya maji, waliahidiwa barabara ya lami tangu miaka saba iliyopita lakini hadi sasa hawana hata kipande kidogo tu cha barabara hiyo. Shabani Mkwimbi ambaye alipewa nafasi ya kuzungumza kwa niaba ya wananchi wenzake, alisema kata hiyo ina kituo cha polisi na mahakama lakini utendaji kazi wa viongozi waliopo hapo unatia shaka.

“Waziri Mkuu tunataka ukimaliza kuzungumza na sisi, uondoke na Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Miono, Maro na msaidizi wake Rashidi pamoja na Hakimu wa hapa, kwa sababu hawa watu habari yao ni nyingine.

Mkulima akienda polisi au mahakamani hashindi kesi hata siku moja, lakini mfugaji akienda anashinda,” alisema huku akishangiliwa. Aliongeza kuwa, “ hawa watu wanadai wana fedha na wanafanya chochote wanachotaka, na ndiyo maana hawalali polisi hata kama wameua mtu.”

Akijibu kero zao, Waziri Mkuu aliwahakikishia wakazi hao kwamba Serikali iliyopo madarakani ni yao na hakuna hata mtu mmoja ambaye yuko juu ya Sheria. Alisema suala la polisi wa kituo cha Miono litashughulikiwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, ambaye alikuwepo katika msafara wake.

“Tena Mkuu wa Mkoa yuko hapa na yeye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huu, atasimamia hilo.” Akifafanua kuhusu suala la wafugaji kuwapiga wakulima, Waziri Mkuu alisema msimamo wa Serikali ni kuwaona wakulima wanafanya kazi zao kwa uhuru na wafugaji nao wanafanya kazi zao kwa uhuru.

Aliwataka maofisa mifugo wa mkoa huo waende kwa wafugaji na kutambua mifugo waliyonayo na kama kuna maeneo wahakikishe wanapatiwa maeneo rasmi .

Aliwataka wafugaji wanaokata mabomba ya maji ya mradi wa maji wa Chalinze (CHALIWASA) ili kupata maji ya kunywesha mifugo yao, waache tabia hiyo mara moja na akaonya kuwa watakaokamatwa, wachukuliwe hatua za kisheria mara moja.
Wafugaji wakorofi wakamatwe na kuchukuliwa hatua, Waziri mkuu Wafugaji wakorofi wakamatwe na kuchukuliwa hatua, Waziri mkuu Reviewed by Zero Degree on 4/03/2017 11:29:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.