Loading...

Watoto marufuku kuchunga mifugo

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe akitoa zawadi kwa mwalimu mkuu wa shule ya msingi Tewe iliyokuwa ya kwanza kiwilaya na ya sita kimkoa katika hafla ya kutunuku zawadi kwa shule zilizofanya vyema katika kilele cha Wiki ya Elimu.
MKUU wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, Godwin Gondwe amewapongeza walimu na wadau wengine wa elimu kwa kazi nzuri wanazofanya katika kuhakikisha wilaya hiyo inazidi kupaa katika elimu huku wanafunzi wakipata elimu bora.

Ametoa kauli hiyo katika hafla ya kutoa zawadi kwa shule 10 za msingi na moja ya sekondari kwa kufanya vizuri kwenye mitihani ya darasa la saba na kidato cha nne 2016.

Shule za msingi zilizopata zawadi na pongezi ni Tewe iliyokuwa ya sita kimkoa na kuzawadiwa Sh 200,000, Chang’ombe Sh 150,000, Mkumba Sh 100,000, Mzundu Sh 82,000, Kwaragulu, Mbwewe, Kwamdani, Kwedikwazu Magharibi, Kwedikwazu Mashariki na Chogo ambazo zote zilipata Sh 78,000.

DC Gondwe aliwataka wakuu wa shule na maofisa elimu kata kusimamia haki ya msingi ya wanafunzi kupata elimu wanayostahili.

Pamoja na kutoa pongezi kwa wanaofundisha na wadau wengine, amepiga marufuku watoto walio na umri wa kuwepo shuleni kuchunga mifugo siku za shule.

Aliwaonya wazazi na jamii ya wafugaji ambao wanakwamisha watoto kupata haki yao ya msingi ya kupata elimu na kwamba sheria itachukua mkondo wake kwa yeyote atakayebainika kwenda kinyume.

Aliwaeleza pia wazazi ambao wana watoto waliovuka umri wa kwenda shule kupelekwa kwa utaratibu wa MEMKWA.

Akizungumzia changamoto zinazowapata walimu, alisema atahakikisha fedha zinazohusu madai ya walimu zinapofika halmashauri zinawafikia walengwa kwa wakati uliopangwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, William Makufwe alisema kukosekana kwa chakula cha kutosha shuleni, utoro uliokithiri kwa baadhi ya wanafunzi, kutokuwajibika kwa baadhi ya walimu na wazazi pamoja na upungufu wa walimu kunasababisha kushuka kwa ufaulu wa wanafunzi.

Aliziagiza shule ambazo mpaka sasa hazina chakula kuhakikisha wanawapa wanafunzi chakula.

Aliwataka pia kusimamia mazao ya mihogo waliyopanda ili mazao hayo yaweze kusaidia upatikanaji wa chakula shuleni na kuongeza kiwango cha uelewa kwa wanafunzi.

Alitoa mwezi mmoja hadi kufikia Mei 4, mwaka huu kwa maofisa watendaji kata, vijiji, walimu wakuu, wakuu wa shule na maofisa elimu kata kuhakikisha kuwa watoto wanapata chakula cha mchana shuleni.
Watoto marufuku kuchunga mifugo Watoto marufuku kuchunga mifugo Reviewed by Zero Degree on 4/06/2017 03:54:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.