Loading...

Waziri Simbachawene amemtumbua Ofisa Elimu Msingi

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene, amemtumbua Ofisa Elimu Msingi, Scolastica Kapinga, kutokana na kutopeleka walimu katika Shule ya Msingi Mbalawala, iliyopo Manispaa ya Dodoma.

Hatua hiyo imechukuliwa siku chache baada ya wazazi kulazimika kuifunga shule hiyo ambayo inadaiwa kuwa na wanafunzi 922 na walimu watatu.

Akizungumza na wazazi na walezi wa wanafunzi wa shule hiyo, Waziri Simbachawene alisema Serikali haiwezi kumvumilia ofisa elimu huyo ambaye ameshindwa kusimamia sekta ya elimu.

Kutokana na hali hiyo, Simbachawene alimwagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Godwin Kunambi, kupeleka walimu 10 shuleni hapo, ndani ya wiki mbili.

“Mkurugenzi nakuagiza ndani ya wiki mbili, kuwe na walimu zaidi ya 10 hapa shuleni kwani haiwezekani shule iliyoko mjini ikose walimu.

“Kwa kuwa shule hii imefungwa, naagiza shule hii ifunguliwe na wazazi lazima mfuatilie maendeleo ya masomo ya watoto wenu,” alisema Simbachawene.

Kwa upande wake, Mbunge wa Dodoma Mjini, Antony Mavunde, alisema ukosefu wa walimu umekuwa ni changamoto kwao na kwamba zinahitajika nguvu za ziada kuwa na idadi kubwa ya walimu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Cristina Mndeme, alisema suala la idadi ya walimu linatakiwa kuangaliwa kwa umakini kwani linaathiri masomo ya wanafunzi.

Source: Mtanzania
Waziri Simbachawene amemtumbua Ofisa Elimu Msingi Waziri Simbachawene amemtumbua Ofisa Elimu Msingi Reviewed by Zero Degree on 4/11/2017 01:46:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.