Loading...

Zitto atoa ufafanuzi juu ya habari inayodai kuwapo kwa ugomvi kati ya ACT na Chadema

''Kuna habari zimetoka leo kwenye Gazeti la Mtanzania zinaeleza kwamba ACT Wazalendo tuna ugomvi na Chadema, wakirejea suala la Uchaguzi wa Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki. Nikiwa kama mwanachama kindakindaki wa ACT Wazalendo, Naomba kutoa maoni yangu kama ifuatavyo:-

Ukweli ni kwamba ACT Wazalendo Hatuna ugomvi na chama chochote. Kitu pekee tunachodai ni haki yetu kama Chama, haki ya kushiriki na kushindana kwenye uchaguzi wa Ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki ili kupitia ushindani huo nchi yetu ipate wawakilishi wazuri na mahiri watakaokwenda kuwa msaada mkubwa katika ujenzi wa Jumuiya na nchi yetu.

Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kifungu cha 50(1) kinatoa ufafanuzi juu ya upatikanaji wa Wabunge wa EALA. 

Moja ya matakwa ya kifungu hicho ni kwamba upatikanaji wa wabunge hao (ambao kwa idadi ni 9 kutoka kila nchi mwanachama) sharti uzingatie uwakilishi wa vyama mbalimbali vya siasa vyenye uwakilishi katika bunge la nchi mwanachama, makundi ya watu wenye maoni tofauti tofauti katika nchi mwanachama, jinsia, na makundi mengine yenye maslahi mbalimbali katika nchi mwanachama.

Sasa, utaratibu uliotolewa na Spika wa Bunge la Tanzania kuwa ndio utakaofuatwa katika kupata wabunge wa EALA, si tu kwamba umekiuka matakwa ya Mkataba wa Jumuiya hivyo kunyima fursa baadhi ya makundi stahiki katika nchi kuweza kushiriki kupata uwakilishi EALA, lakini UMEPOKONYA HAKI YETU SISI CHAMA CHA ACT WAZALENDO ya kushiriki katika uchaguzi huo. 

Chama cha ACT Wazalendo kina uwakilishi ndani ya Bunge, na Mkataba umetaka vyama vyenye uwakilishi vipate fursa ya kushiriki kutafuta wawakilishi wa Bunge la Afrika Mashariki. Mkataba haujasema kuwa Chama chenye mwakilishi mmoja basi kisishiriki uchaguzi!! Mwongozo wa Spika unatupatia sisi ACT Wazalendo fursa ya kupiga kura (kuchagua) lakini hautupatii haki ya kupigiwa kura (kuchaguliwa). 

Hilo ndilo tunalopinga. Tunapinga 'ugawanaji' wa viti badala ya kufanya uchaguzi ili wenye sifa, uwezo na vigezo washinde. Wala hatugombani na chama chochote.

*Kiongozi wa Chama chetu ambaye pia ni mbunge katika Bunge la Jamhuri amekwisha mwandikia Spika Barua akimkumbusha juu ya haki yetu ya msingi kushiriki uchaguzi wa EALA, na amewasilisha mapendekezo katika Kamati ya Kanuni ambayo tunaamini yatatuongoza kutenda haki na kufikia adhma ya kushiriki, kushindana na hatimaye kupata wawakilishi wenye 'mashiko' katika Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki. ACT Wazalendo, tunaye mgombea bora na mahiri kabisa kabisa katika nafasi hiyo. Tusizibiwe fursa kwa sababu zisizokuwa sababu!!

Mapendekezo Mahususi kuhusu Kundi C ( vyama vya Upinzani ) kwenye Uchaguzi wa wawakilishi wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki ( EALA )

Napendekeza kwamba wawakilishi wa Kundi C ( vyama vya Upinzani ) wagawanywe Kwenye Makundi 2 kama ifuatavyo;

KUNDI C liwe na C-1 na C-2

C-1 Nafasi 1 ambayo wagombea watapendekezwa na Chama Kikuu cha Upinzani Bungeni na kupigiwa kura na Bunge zima.

C-2 Nafasi 2 ambazo wagombea wake watapendekezwa na Vyama vyote vya Upinzani Bungeni na kupigiwa kura na Bunge zima

Kwa mapendekezo hayo Chama Kikuu cha Upinzani Bungeni kwa sasa ( CHADEMA ) kitakuwa na uhakika wa kuwa na mbunge EALA na vyama vingine vitakuwa na haki ya kugombea katika uchaguzi huu.

Nawasilisha kwa hatua za haraka kwa maslahi ya Tanzania.''


Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto , MB

Kigoma Mjini

Mapendekezo yetu kwenye Kamati ya kanuni ni hayo hapo. Hatuna ugomvi na CHADEMA bali tunataka haki yetu ya kugombea.

Kupitia Ukurasa wake wa Facebook, Zitto kabwe ameandika hivi:

Zitto atoa ufafanuzi juu ya habari inayodai kuwapo kwa ugomvi kati ya ACT na Chadema Zitto atoa ufafanuzi juu ya habari inayodai kuwapo kwa ugomvi kati ya ACT na Chadema Reviewed by Zero Degree on 4/01/2017 03:50:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.