Loading...

Bunge haliwezi kuendeshwa na taarifa za magazeti, Chenge

MWENYEKITI wa Bunge, Andrew Chenge (pichani), amesema Bunge haliwezi kuendeshwa kwa taarifa za magazeti, bali kwa kuzingatia taratibu na kanuni zake.

Chenge alisema hayo jana bungeni Dodoma baada ya Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema) kuomba mwongozo wa spika akitaka kufahamishwa juu ya taarifa alizosema zinasambaa katika magazeti na mitandao ya kijamii kuwa, fedha walizochangia kwa ajili ya rambirambi zimetumiwa kwa matumizi mengine.

Akijibu muongozo huo, Chenge ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi (CCM) aliwataka wabunge kuwa na imani kuhusu suala hilo kwani Serikali pamoja Bunge wote wapo na wanalifuatilia suala hilo. “Serikali ipo, Bunge hili lipo, Uongozi wa Bunge upo, na tunategemea kupata mrejesho wa michango ya Bunge ili siku za usoni mtakapokuja kuombwa kufanya hivyo, muwe na uhiari wa kuchangia kwa haraka,” alisema. Hata hivyo, alimtaka Waitara akumbuke kuwa Bunge hilo haliendeshwi na magazeti.


“Kwa heshima zote na kwa mila zetu, ukishatoa mchango wako wa rambirambi, unaiachia familia ile au chombo kile hayo yanakwisha. Ukianza kuleta tuhuma kwamba fedha hazijaenda huko, mimi nasema kidogo ni tatizo… kwa kuwa hilo halijatokea bungeni,” alisema. 

Chenge alisema Bunge hilo linasubiri mrejesho wa fedha za rambirambiya Sh milioni 100 ya Bunge iliyopelekwa kwenye msiba wa watoto wa Shule ya Msingi Lucky Vicent, waliofariki kwa ajali ya gari jijini Arusha.

Mei 6, mwaka huu, wanafunzi 32 wa darasa la saba, walimu wao wawili na dereva wa shule hiyo walifariki katika ajali ya gari iliyotokea katika eneo la Rhotia, Karatu, mkoani Arusha. Kutokana na ajali hiyo, Watanzania mbalimbali wakiwemo wabunge walichangia fedha kufanikisha maziko ya miili ya watu hao. Wabunge kwa hiari yao walichangia kupitia posho zao za siku moja na kupeleka rambirambi ya Sh milioni 86, lakini pia kupitia Ofisi ya Spika Bunge liliongeza Sh milioni 14 na kufanya jumla ya rambirambi kuwa Sh milioni 100.

Chenge alitoa taarifa hiyo ya Bunge kusubiri mrejesho wa rambirambihizo bungeni Dodoma jana baada ya mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema) kuomba mwongozo wa spika akitaka kufahamishwa juu ya taarifa zinazodai kuwa fedha walizochangia kwa ajili ya rambirambi zimetumiwa kwa matumizi mengine.

Awali wakati akiomba mwongozo wa spika, Mbunge Waitara alisema magazeti kadhaa aliyosoma jana yalielezea kuwa, badala ya fedha walizochanga wabunge na wananchi wengi kama rambirambi kwa msiba huo kutumika kwa wafiwa na walioathirika na msiba huo, zinadaiwa kutumika kwa ajili ya kukarabati hospitali.

Aidha, Waitara alisema kwa mujibu wa magazeti hayo, fedha hizo zimedaiwa pia kutumika kuwalipa madaktari walioenda na watoto majeruhi Marekani kwa ajili ya kutibiwa kama posho. Aliomba mwongozo wa Spika na kutaka wabunge kutaarifiwa kama kitendo hicho cha fedha za rambirambi kutumika kufanyia mambo mengine badala ya kuwafariji wafiwa ni sahihi au la.

Kutokana na ajali hiyo, wanafunzi walionusurika Wilson Tarimo, Sadya Awadh na Doren Elibariki hivi sasa wapo nchini Marekani kwa ajili ya matibabu huku hali zao zikiendelea kuimarika. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo aliratibu ukusanyaji wa fedha hizo. Zaidi ya Sh milioni 300 zilipatikana huku akieleza kuwa, Sh milioni 109 zilitumika kununua majeneza 35 na kusafirisha miili iliyoagwa kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid na kuipelekwa ilipotakiwa kuzikwa.

Credits: Habari Leo
Bunge haliwezi kuendeshwa na taarifa za magazeti, Chenge Bunge haliwezi kuendeshwa na taarifa za magazeti, Chenge Reviewed by Zero Degree on 5/23/2017 11:15:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.