Loading...

Hakimu ajitoa kusikiliza kesi kisa rafiki zake

HAKIMU Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Ajali Milanzi amejitoa kusikiliza kesi inayowakabili viongozi watatu wa serikali ya kijiji cha Isenegeja, kata ya Mwisi, ya wizi wa sh. milioni 34.1 za serikali.

Milanzi alisema hawezi kuendelea kusikiliza kesi hiyo kwa sababu baadhi ya wadhamini wa washtakiwa ni marafiki zake hivyo ameona anaweza kushindwa kutenda haki.

Baada ya hakimu Milanzi kuwasilisha kusudio la kujitoa, upande wa mashitaka ukiongozwa na mwendesha mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Edson Mapalala akishirikiana na wakili wa serikali, Tumaini Pius walikubaliana nalo na kuomba mahakama kuondoa kesi hiyo.

Baada ya mahakama kuiondoa kesi hiyo, washtakiwa wote watatu: Ahmed Jambeck, Seleli Kashindye na Michael John walikamatwa tena na maofisa wa Takukuru wakati wakitoka nje ya mahakama hiyo.

Walipakiwa kwenye gari kisha kupelekwa mjini Tabora.

Baada ya kufikishwa Tabora walifunguliwa kesi upya katika Mahakama ya Hakimu Mkazi.

Awali mwendesha mashitaka wa Takukuru, Mapalala aliiambia mahakama mbele ya Hakimu Mkazi, Emmanuel Ngigwaana kuwa washtakiwa wote watatu, Jambeck(50) ambaye ni mwenyekiti wa kijiji, Seleli Kashindye(58) mjumbe na Michael John (47) aliyekuwa kaimu mtendaji wa kijiji hicho, wanakabiliwa na makosa mawili.

Mapalala aliiambia mahakama kosa la kwanza ni wizi wa fedha wakiwa watumishi wa serikali ya kijiji cha Isenegeja.

Kosa la pili, alisema ni wizi ambapo kati ya mwaka 2008 hadi 2015 wakiwa watumishi katika kijiji hicho, kwa pamoja waliiba fedha kiasi cha milioni 34.131.

Aidha, mwendesha mashtaka huyo aliendelea kuiambia mahakama kuwa baada ya washtakiwa kufanya wizi huo walibadilisha kwa matumizi yao binafsi bila kuwa na haki yoyote.

Washtakiwa wote watatu walikana kutenda makosa hayo.

Watuhumiwa hao walipewa masharti ya dhamana kuwa kila mtuhumiwa mmoja kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika ambao watasaini bondi ya sh. milioni saba, ambayo walitimiza.

Kesi itaanza kusikilizwa Jumatano ijayo baada ya upelelezi kuelezwa kuwa umekamilika.
Hakimu ajitoa kusikiliza kesi kisa rafiki zake Hakimu ajitoa kusikiliza kesi kisa rafiki zake Reviewed by Zero Degree on 5/09/2017 11:08:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.