Loading...

Mume alivyoua mkewe kwa kumpiga risasi kisha na yeye kujimaliza

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi.
MKAZI wa Kata ya Kanyerere Wilaya ya Nyamagana, mkoani Mwanza, Maximilian Ngedere, amemuua mkewe kwa kumpiga risasi kisha na yeye kujimaliza kwa risasi kama alivyomuua mkewe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, akisema kwamba lilitokea saa 4:30 usiku kwa wanandoa hao ambao wote ni wafanyabiashara wa samaki mkoani hapa.

Alisema kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, majirani walianza kusikia wanandoa hao wakibishana chumbani kwao na ndipo ghafla walisikia milio ya risasi na kuamua kutoa taarifa polisi.

Kamanda Msangi alisema majirani baada ya kusikia ukimya waliingia kwenye nyumba hiyo kutaka kujua kinachoendelea na ndipo walipomkuta mwanamke huyo aliyefahamika kwa jina la Teddy Patrick akigalagala sakafuni huku akiomba msaada.

Alisema mwanamke huyo alikuwa amepigwa risasi sehemu ya mgongoni na kutokezea tumboni na kwenye paja la mguu wa kulia.

“Walimkuta anagalagala chini akiomba msaada wa kupelekwa hospitali na wakati huo huo walikuta yule mwanaume akiwa ameanguka chini… alikuwa amejipiga risasi kifuani kushoto karibu na moyo na bastola yake ilikuwa pembeni, “ alisema Kamanda Msangi 

Kamanda Msangi alisema wasamaria wema walimbeba mwanamke huyo na kumpeleka hospitali ya Bugando lakini alifariki wakati akiendelea kupatiwa matibabu.

Alisema mwanaume huyo alitumia bastola aina ya Lami BJ30666 yenye namba za 00103129 iliyokutwa pembeni ya kitanda wakati huo akiwa tayari ameshakufa.

“Chanzo cha tukio hakijafahamika vizuri, lakini kuna watu wanasema inaonekana kama vile walitofautiana kuhusu jambo fulani,” 

Alisema yalikutwa maganda matatu ya risasi na moja ambayo ilikuwa haijalipuka wakati kwenye magazine kulikutwa na risasi mbili. Kamanda Msangi alisema miili ya marehemu wote imehifadhiwa kwenye hospitali ya Bugando na uchunguzi ukikamilika ndugu wataruhusiwa kuchukua miili yao.
Mume alivyoua mkewe kwa kumpiga risasi kisha na yeye kujimaliza Mume alivyoua mkewe kwa kumpiga risasi kisha na yeye kujimaliza Reviewed by Zero Degree on 5/27/2017 11:53:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.