Loading...

Mvua ilivyosababisha hasara ya zaidi ya milioni 700 mkoani Katavi

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Raphael Muhuga
MKUU wa Mkoa wa Katavi, Raphael Muhuga, amesema hasara halisi iliyosababishwa na mvua kubwa iliyoabatana na upepo mkali iliyonyesha katika kijiji cha Kasansa kilichopo katika wilaya ya Mlele imefikia zaidi ya Sh milioni 780.

Aidha, mvua hiyo iliyonyesha mapema mwaka huu ilisababisha vifo vya watoto sita akiwemo mtoto mwenye umri wa wiki na watatu wa familia moja ambapo ilibomoa nyumba za makazi zipatazo 42. 

Muhuga alisema timu ya wataalamu aliyoiunda imetoa taarifa ya tathmini ya maafa hayo yaliyosababishwa na mvua iliyosababisha mafuruko makubwa katika kijji cha Kasansa kwamba hasara halisi ni Sh 709,780,041. 

Akifafanua alisema tathmini inaonesha kuwa hasara halisi ya uharibifu wa miundombinu ikiwemo ya miradi ya umwagiliaji na barabara iliyosababishwa na mvua hiyo ni Sh 591,228,041, thamani ya uharibifu wa mazao ni Sh 89,562,041 na vifaa na mali vya thamani ya Sh 28,9990,000 viliharibiwa.

“Maafa yaliyosababishwa na mvua hiyo ni makubwa kwani watoto sita walipoteza maisha yao huku nyumba 42 zilibomolewa tathmini inaonesha kuwa pia mradi mkubwa wa umwagiliaji uliopo katika kijiji cha Kilida, wilayani Mlele ambao ujenzi wake ulikuwa umekamilika kwa asilimia 100 umeharibiwa vibaya zaidi ya Sh milioni 450 zinahitajika kwa ajili ya ukarabati wa mradi huo. Pia mradi wa maji uliokuwa ukisambaza maji katika vijiji vya Kasansa na Kilida umeharibiwa vibaya na kusababisha adha kubwa kwa wakazi wa vijiji hivyo,” alieleza. 

Aliongeza kuwa tayari Kanisa la PEFA lililopo katika wilaya ya Mlele limetoa msaada wa vifaa vya ujenzi yakiwemo mabati bando 24 kwa familia 24 zilizoathirika kwa kukosa makazi ya kudumu ukiwa na thamani ya zaidi ya Sh milioni 22.4.

“Serikali kupitia kitengo chake cha maafa kimetoa msaada wa vitanda 46, magodoro 46, na shuka 46 lakini msaada huo bado hatujaupokea lakini gharama za usafirishaji ni jukumu letu sisi Serikali ya mkoa,” alieleza. 

Watoto sita waliopoteza maisha yao watano miongoni mwa walikuwa wakiishi na wazazi wao katika kijiji cha Kasansa, kata ya Kasansa huku mwingine wa sita alikuwa mtoto wa mwalimu wa Shule ya Msingi Kilida.

Waliofariki walitambuliwa kuwa ni pamoja na ndugu watatu wa familia moja, Isabela Milambo (14 ) aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la sita, Jane Milambo (10) ambaye alikuwa mwanafunzi wa darasa la nne na Mwasi Milambo (5) ambaye alikuwa hasomi. Wengine ni Revinus Joseph (10), mwanafunzi wa darasa la nne na Anjela Justin, aliyekuwa na umri wa wiki, Leduisi Suwi (6) mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Kilida iliyopo katika kata ya Kasansa ambaye mzazi wake aitwae Moses Suwi anafundisha katika shule hiyo.
Mvua ilivyosababisha hasara ya zaidi ya milioni 700 mkoani Katavi Mvua ilivyosababisha hasara ya zaidi ya milioni 700 mkoani Katavi Reviewed by Zero Degree on 5/10/2017 12:22:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.