Loading...

Polisi walivyozuia mkutano wa Julius Matatiro mkoani Tanga

JESHI la Polisi mkoani Tanga limemzuia Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro kufanya ziara ya siku mbili ya kukagua na kuimarisha shughuli za chama katika Wilaya ya Tanga kwa sababu za usalama.

Mtatiro alitakiwa kuanza ziara hiyo, Mei 6 hadi 7 na alilenga kufanya kikao cha kamati ya utendaji na shughuli za kuimarisha chama ikiwamo kufungua matawi na kupokea wanachama wapya.

Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD), Idi Abdallah, alisema walilazimika kusimamisha ziara hiyo baada ya kupokea taarifa za intelejensia zinazoonyesha kuwapo viashiria vya uvunjifu wa amani.

“Tumepokea taarifa kutoka ndani ya chama kuwa ziara hiyo pamoja na mikutano isingeweza kuisha salama bila kuwapo matukio ya vurugu na umwagaji damu… kulinda amani ya wilaya yetu, tumeona tusimamishe ziara hii,” alisema Abdalla.

Kabla ya msafara wa Mtatiro kuwasili katika ofisi za CUF zilizoko Barabara ya 20, magari ya polisi yalikuwa yakifanya doria nje ya ofisi hiyo kwa ajili ya kulinda usalama.

Baada ya msafara wa kiongozi huyo kufika, uongozi wa wilaya uliombwa Kituo cha Polisi Chumbageni kwa ajili ya kuonana na OCD.

Viongozi wote walitii agizo hilo na kuwasili Chumbageni, ambako walikaa dakika 45 na baadaye kuruhusiwa kurudi kuzungumza na wanachama wao kuhusu maagizo waliyopewa.

Mtatiro aliwaeleza wanachama kuwa wamepewa agizo la kusimamisha shughuli zote ambazo zilikuwa zifanyike katika ziara hiyo kutokana na sababu za usalama.

Alisema wameamua kutii amri ya polisi kuepuka madhara ambayo yanaweza kuwapata wanachama wake.

“Sitaki mapambano ya wananchi na polisi yabakishe makovu na madhara, ninawaahidi nitakuja wakati mwingine hali itakapokuwa sawa kuendelea na majukumu ya kuimarisha chama,” alisema Mtatiro.

Hata hivyo, alitoa maagizo kwa madiwani wa chama hicho kumaliza tofauti zao na kuhakikisha wanaimarisha shughuli za chama ikiwamo kusimamia na kutetea ahadi walizotoa kwa wananchi.

Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Tanga, Rashid Jumbe alisema msimamo wa wanachama katika wilaya hiyo ni kuwa hawaungi mkono vitendo vya uhujumu wa chama vinavyofanywa na Mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba .

Mbunge wa Viti Maalum, Saumu Sakala (CUF), alionyesha kusikitishwa na kitendo cha polisi kuzuia mkutano huo.

Source: Mtanzania
Polisi walivyozuia mkutano wa Julius Matatiro mkoani Tanga Polisi walivyozuia mkutano wa Julius Matatiro mkoani Tanga Reviewed by Zero Degree on 5/08/2017 08:33:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.