Loading...

Rais Zuma aja na neema Tanzania

RAIS Dk. John Magufuli amemwomba Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma kumsaidia namna ya kuzungumza na Umoja wa Nchi tano zinazochipukia katika uchumi (Brics), ili apate mkopo wa riba nafuu utakaosaidia kujenga reli ya kati ya kisasa (Standard Gauge).

Pia amesema wamekubaliana na Rais Zuma kuwa atapeleka walimu wa Tanzania kwenda Afrika Kusini kufundisha Kiswahili.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo Ikulu Dar es Salaam jana wakati wa hafla ya kutia saini mikataba mitatu ya ushirikiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini.

Rais Zuma ambaye yuko nchini kwa ziara ya siku mbili, kabla ya kutiliana saini hizo, aliteta na Rais Magufuli kwa saa takribani mbili.

Hati hizo ni pamoja na muhtasari wa makubaliano ya mkutano wa tume ya pamoja ya marais, makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya bioanuwai na uhifadhi na makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya uchukuzi.

Viongozi hao pia walizindua rasmi Tume ya Pamoja ya Marais (Bi- National Commission- BNC), kwa kufanya kikao cha kwanza cha tume hiyo tangu ianzishwe mwaka 2011, huku wakipokea makubaliano yaliyofikiwa katika kikao cha tume ngazi ya mawaziri.

Akizungumza baada ya utiaji saini huo, Rais Magufuli alisema katika mazungumzo yake na Rais Zuma, alimweleza kuhusu ujenzi wa reli ya kati, mradi wa Liganga na Mchuchuma na kuwataka wafanyabiashara wa nchi hiyo kuwekeza nchini.

“Nimemuarifu Rais Zuma kuhusu miundombinu ikiwa ni pamoja na ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge), mradi wa Liganga na Mchuchuma na nimewakaribisha wawekezaji kutoka Afrika Kusini.

“Nimemwomba kupitia zile nchi zenye utajiri unaoinukia, Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini kutusaidia kupata mkopo wa riba nafuu utakaotusaidia kujenga Standard Gauge. Najua yeye hatashindwa akitia neno.

“Pia tumekubaliana na Rais Zuma kuwa Tanzania itapeleka walimu wa Kiswahili ambacho kinazungumzwa na watu takribani milioni 120 duniani wakafundishe lugha hiyo katika vyuo vya nchi hiyo,” alisema Rais Magufuli.

Alisema kwa kuwa Tanzania imefanya mengi katika ukombozi wa nchi hiyo, hivyo waifikirie namna ya kuisaidia.

Alisema hivi sasa biashara kati ya Tanzania na Afrika Kusini kwa mwaka ni Sh trilioni 2.4, uwekezaji wa Afrika Kusini nchini ni Dola za Marekani milioni 803.15 uliozalisha ajira 20,916 na kwamba kiwango hicho kinaweza kuongezeka.

Pia alimshukuru Rais huyo wa Afrika Kusini kwa mchango wa madawati 1000 yaliyotolewa na Serikali ya nchi hiyo wakati wa kampeni za kuchangia madawati.

Rais Zuma

Naye Rais Zuma alitoa pole kwa Watanzania kuhusiana na ajali iliyosababisha vifo vya wanafunzi 32 wa Shule ya Lucky Vicent, walimu wawili na dereva wa basi mkoani Arusha.

“Napenda kutoa pole kwa vifo vya watoto iliyotokana na ajali huko Arusha. Tunaungana na Watanzania kuwalilia hawa watoto ambao wamepoteza maisha yao wakiwa wadogo,” alisema Rais Zuma.

Rais Zuma ambaye alifuatana na mawaziri sita na wafanyabiashara zaidi ya 80 wa nchi hiyo, alimpongeza Rais Magufuli kwa kuanza ujenzi wa reli ya kati huku akiahidi kuunga mkono juhudi hizo.

Alisema anatambua kuwa ujenzi wa reli ya kati utaleta manufaa makubwa kwa Tanzania na nchi za Maziwa Makuu hivyo atahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji wa nchi yake kushirikiana kufanikisha mradi huo.

“Pia nimefurahi tumekumbuka tulikotoka katika uhusiano wetu, nimekumbuka Mazimbu mkoani Morogoro hatuwezi kusahau pia Dakawa.

“Jana nilipofika wakati natambulishwa viongozi, mmoja akasema katokea Kinondoni nikasema kanikumbusha mbali,” alisema Rais Zuma.

Rais Zuma alimwalika Rais Magufuli kufanya ziara nchini humo kuendelea kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili.

WAFANYABIASHARA AFRIKA KUSINI

Wafanyabiashara kutoka Afrika Kusini wamesema wamewashauri Watanzania kuongeza uzalishaji wa bidhaa na kuuuza nchini mwao kuinua uchumi kati ya nchi hizi mbili.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Uwekezaji Afrika, Kitengo cha Biashara na Viwanda Afrika Kusini, Zanele Mkhize wakati wa mkutano kati ya wafanyabiashara Tanzania na Afrika Kusini, Dar es Salaam jana.

Akieleza umuhimu wa uhusiano wa uchumi endelelvu kati ya nchi hizo mbili, alisema ingawa kwa sasa bado idadi ya wawekezaji Watanzania nchini Afrika Kusini ni ndogo, ipo haja ya wengine kuendelea kuwekeza nchini humo.
Rais Zuma aja na neema Tanzania Rais Zuma aja na neema Tanzania Reviewed by Zero Degree on 5/12/2017 11:04:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.