Loading...

Serengeti Boys yapata udhamini kutoka kampuni ya SportPesa

SportPesa ni moja ya makampuni yanayoidhamini klabu ya Hull City inayocheza Ligi ya Uingereza
Timu ya Tanzania ya soka ya wachezaji chipukizi, Serengeti Boys Jumanne wiki hii imepata udhamini wa $22,000 kutoka kwa kampuni ya SportPesa.

Kampuni hiyo ilitangaza udhamini huo wakati ikizindua rasmi huduma ya uchezaji wa kamari kwa kubashiri mechi za kandanda nchini Tanzania.

Waziri wa Mawasiliano, Utamaduni na Michezo nchini Tanzania Harrison Mwakyembe, akizungumza Dar es Salaam wakati wa uzinduzi huo, amesema wanakaribisha SportPesa nchini Tanzania sio kuendeleza michezo tu lakini kuanzisha miradi ambayo itawezesha raia wa nchi hiyo kupata ajira.



"Ninawahakikishia ushirikiano wetu, karibuni kwa nchi hii ya michezo,'' amesema Mwakyembe, na kuongeza: "Huu ndio wakati mwafaka wa kuendeleza michezo humu nchini tukiwa na wenzetu wa SportPesa ambao nina hakika wataendeleza michezo mingine pia sio kandanda pekee.''

Mkurugenzi wa usimamizi wa kampuni ya SportPesa nchini Tanzania, Abbas Tarimba amesema haya: "Tunanuia kubadilisha sura ya michezo nchini Tanzania. Naomba wananchi wa Tanzania muwe watulizu hadi Jumamosi tutakapotangaza rasmi ni timu zipi zitadhaminiwa na SportPesa.


"Tanzania ina wachezaji wengi wana vipaji (kama Mbwana Samatta), na miezi michache ijayo tuna mipango ya kuanzisha miradi mikubwa ya kandanda.''

Mkurugenzi kaimu wa mamlaka ya uchezaji kamari nchini Tanzania, James Mbawe, ametangaza rasmi SportPesa wamepewa leseni ya kamari baada kutimiza masharti yao yote.

Amesema Mbawe: "Uchezaji kamari kupitia michezo umepiga hatua kubwa nchini Tanzania na kuletea taifa letu mapato zaidi ya dola milioni tisa mwaka wa 2015 na 2016.

"Miaka minne iliyopita wenyeji walikua wanatizama kandanda kujifurahisha lakini sasa watu wanatizama na kutabiri matokeo ya mpira wa miguu, na hii imewapa vijana ajira na kuendeleza miradi ya kijamii.''
Serengeti Boys yapata udhamini kutoka kampuni ya SportPesa Serengeti Boys yapata udhamini kutoka kampuni ya SportPesa Reviewed by Zero Degree on 5/10/2017 12:47:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.