Tamisemi kuajiri walimu kufidia pengo la waliokumbwa na sakata la vyeti feki
WIZARA ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imesema inaendelea na uhakiki wa walimu wangapi wa shule za msingi na sekondari, ambao wamepatikana na vyeti feki ili kuajiri walimu wapya watakaoziba pengo lililopo.
Akizungumza jana Dar es Salaam katika mahafali ya kidato cha sita ya Shule za Sekondari za Feza, Naibu Waziri Tamisemi, Suleiman Jafo alisema kuwa katika uhakiki wa watumishi wa umma wenye vyeti feki, sekta ya elimu kwa upande wa walimu na sekta ya afya ndio imeonekana kuwa na watumishi wengi walioghushi vyeti.
Jafo alisema kuwa baada ya tathmini hiyo, wataipeleka katika wizara husika ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa ajili ya kupitia ili katika mwaka ujao wa fedha waweze kuajiri walimu wapya kuziba pengo lililopo.
“Katika uhakiki wa vyeti feki ni kweli kwamba sekta ya elimu na afya ndio imeongoza kwa kuwa na watumishi wengi wenye vyeti feki hivyo tunaendelea na tathmini nchi nzima ili kujua ni walimu wangapi wa shule za msingi na sekondari waliokutwa na vyeti hivyo,” alisema Jafo.
Aidha, alisema serikali inaendelea kufanya maboresho katika shule kongwe za sekondari kwa ajili ya kupandisha kiwango cha elimu nchini. Alisema kuwa wameanza ukarabati wa shule hizo ambapo tayari wametoa Sh bilioni moja kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya shule 32 za sekondari ikiwa ni pamoja na shule zinazotoa elimu ya kidato cha tano na cha sita.
“Kwa upande wa kidato cha tano na cha sita kwa shule za serikali, zimeanza kuaminika kwani wazazi wengi wanawapeleka watoto wao licha ya kwamba mara nyingi wanafunzi hao wanaanzia katika shule binafsi. Kutokana na hali hii serikali inawekeza katika shule kongwe kwa ajiliya kuboresha miundombinu yake,” alifafanua Jafo.
Pia aliongeza kuwa serikali imetoa Sh bilioni 64 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na walimu na kwamba imetoa Sh bilioni 16 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya maabara kwa shule za sekondari.
Katika mpango wa elimu bure, Jafo alisema serikali awali ilikuwa inatoa Sh bilioni 18.7 kwa ajili ya kulipa posho za walimu wakuu wa shule za msingi, sekondari na waratibu elimu lakini kwa sasa wanatoa Sh bilioni 22 kwa kila mwezi kufanikisha mpango huo.
Katika mpango wa elimu bure, Jafo alisema serikali awali ilikuwa inatoa Sh bilioni 18.7 kwa ajili ya kulipa posho za walimu wakuu wa shule za msingi, sekondari na waratibu elimu lakini kwa sasa wanatoa Sh bilioni 22 kwa kila mwezi kufanikisha mpango huo.
Hata hivyo, aliwataka wahitimu kuhakikisha kwamba wanakuwa chachu ya maendeleo ya taifa kwa kupinga matumizi ya dawa za kulevya, ufisadi na rushwa kwa kuwa serikali inategemea vijana wenye elimu watakaopambana na changamoto hizo.
Alisema itakuwa ni jambo la kushangaza kuona wanafunzi ambao wazazi wamewagharamikia kwa kiasi kikubwa kuishia katika matumizi ya dawa za kulevya na ujambazi badala ya kuleta mapinduzi ya kimaendeleo nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) Profesa Yunus Mgaya alisema kuwa hiyo hatua ya kuhitimu kwa wanafunzi hao, ni mwanzo wa kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) Profesa Yunus Mgaya alisema kuwa hiyo hatua ya kuhitimu kwa wanafunzi hao, ni mwanzo wa kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Profesa Mgaya alisema huo ni mwanzo wao kuelekea katika masomo ya elimu ya juu kupitia fani mbalimbali kwani wanaamini kwamba shule hiyo imewafundisha vyema ikiwa ni pamoja na masuala ya uongozi, nidhamu na namna ya kukabiliana na changamoto.
“Kama mzazi nategemea kuwa tutapata wanafunzi bora katika shule hii, naomba muendelee kujiamini kwamba mnaweza na mumtangulize Mungu katika kila jambo kwani mtafanikiwa,” alisema Profesa Mgaya.
Tamisemi kuajiri walimu kufidia pengo la waliokumbwa na sakata la vyeti feki
Reviewed by Zero Degree
on
5/22/2017 07:16:00 PM
Rating: