Loading...

Vinara wa kutoa wachezaji bora wa mwezi Ligi Kuu ya Vodacom [VPL]

PAZIA la Ligi Kuu Tanzania msimu wa 2016/17 limefungwa rasmi jana kwa timu zote 16, ambapo kila timu imevuna kile ilichopanda kwa msimu mzima.

Tumeshuhudia ushiriki wa timu zote huku kila moja ikijaribu kuendana na mikakati iliyojiwekea kwa kipindi chote cha maandalizi yake na kupelekea kupata matokeo ya kile walichotarajia.

Mbali na ushindani ulioonyeshwa na timu shiriki, pia yapo mambo mbalimbali yaliyonogesha na kuongeza msisimko kwenye ligi hiyo sambamba na mapungufu ambayo ni sehemu ya matukio yaliyoweza kujitokeza wakati ligi hiyo ikiendelea.

Ukiachilia vigogo wa soka Simba na Yanga, pia msimu huu timu ya Kagera Sugar imeingia kwenye rekodi mpya baada ya kucheza soka lenye malengo ambalo limewaweka kwenye ramani ya ushindani huku ikiwanyima usingizi vigogo hao wa soka hapa nchini.

Tumeshuhudia mbali ya ushindani ulioonyeshwa na baadhi ya mastaa, lakini klabu za Simba na Kagera Sugar ndizo zilizoongoza kwa kutoa wachezaji bora zaidi ya mmoja ambao hupatikana kila mwezi kutokana na uwezo wao uwanjani.

Katika tuzo hiyo ambayo hutolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), huangalia uwezo wa mchezaji husika kutokana na mchango wake ndani ya klabu yake sambamba na nidhamu, hawa ndio wachezaji walioweza kufanya vizuri kwa msimu mzima tangu tuzo hizo zianze kutolewa.

Method Mwanjali-Simba

Huyu ni beki kisiki wa Simba ambaye alichaguliwa kuwa mchezji bora wa mwezi Desemba mwaka jana, baada ya kuonyesha uwezo mkubwa akiwa na klabu yake.

Haikuwa kazi rahisi kwa Mwanjali kushinda nafasi hiyo kwa kuwa alikuwa akiwania nafasi hiyo na wachezaji wakali zaidi akiwamo kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima na mlinzi wa kati wa Azam, Yakubu Mohammed.

Mwanjali aliiongoza Simba kushinda michezo mitatu ndani ya mwezi huo, hivyo timu yake kupata ushindi wa asilimia 100 kwa kunyakua alama zote tisa na kusalia nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa ligi nafasi ambayo walikuwa nayo wakati wanaingia raundi ya 16.

Pia katika raundi hizo Simba haikufungwa bao hata moja, huku Mwanjali akicheza kwa dakika zote 270 bila kuoneshwa kadi yoyote akichangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya timu yake huku akijinyakulia kitita cha shilingi milioni moja.

Shiza Kichuya-Simba

Klabu ya Simba haikujuta kumsajili mshambuliaji wao Shiza Kichuya aliyetokea Mtibwa Sugar kutokana na kiwango chake alichokionyesha, huku akionekana kuwasumbua sana wapinzani mara tu wanapokutana naye.

Ubora wa Kichuya pia ulidhihirishwa na TFF pale ilipoona mchango wake akiwa na klabu yake ambapo alifanikiwa kupata tuzo ya mchezaji bora wa mwezi Septemba, ambapo alikuwa akishindanishwa na Adam kingwande pamoja na Omar Mponda wa Ndanda FC.

Kichuya aliisaidia timu yake kupata pointi 12 kwa mwezi huo katika michezo minne aliyocheza matokeo yaliyoifanya klabu yake iendelee kuongoza ligi na pia alifunga mabao matatu katika mechi mbili kati ya nne alizocheza.

Mbaraka Yusuph-Kagera Sugar

Kiwango kilichoonyeshwa na kinda huyu wa Kagera Sugar msimu uliomalizika hakina shaka kuwa kimewagusa mashabiki wengi wa soka hadi kuanza kufuatiliwa na vigogo wa soka hapa nchini kwa lengo la kuhitaji huduma yake msimu ujao.

Mbaraka Yusuph ametajwa kuwa miongoni mwa wachezaji walioweza kuonyesha kandanda safi na la kuvutia hadi kuwashawishi viongozi wa TFF kumpa tuzo ya mchezaji bora wa mwezi Machi kutokana na juhudi zake uwanjani.

Kinda huyo alifanikiwa kuwashinda wenzake Aboubakar Salum ‘Sure Boy’ wa Azam na Kenny Ally wa Mbeya City.

Katika mwezi huo ilichezwa raundi moja tu na Mbaraka ambaye alicheza kwa dakika zote 90, aliisaidia timu yake kukusanya pointi zote tatu zilizoifanya timu yake kubaki katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi kwa mwezi huo huku akifunga goli moja na kuonyesha nidhamu ya hali ya juu.

Juma Kaseja- Kagera Sugar

Kaseja alisajiliwa na Kagera Sugar sambamba na kocha wake Mecky Mexime, ambapo ujio wao umezaa matunda ndani ya klabu ya Kagera kutokana na kiwango kikubwa walichokionyesha na kujikuta wakiwa katika timu za juu kwenye msimamo wa ligi.

Golikipa huyo mkongwe ambaye alizichezea Simba na Yanga kwa mafanikio, ameendelea kuwa chachu ya mafanikio ndani ya Kagera kwani licha ya kuchaguliwa mchezaji bora wa mwezi Januari pia ameonyesha nidhamu ya hali ya juu sana.

Kaseja aliwashinda wachezaji wenzake Mbaraka Abeid wa Kagera Sugar na Jamal Mtengeta wa Toto African na kufanikiwa kuchukua kitita cha milioni moja.

Katika mechi tatu ambazo timu ya Kagera ilicheza kwa mwezi huo, Kaseja ambaye alicheza kwa dakika zote 270 alikuwa kiongozi na mhimili wa timu na aliisaidia timu yake kupata ushindi katika michezo yote ambapo ilikusanya jumla ya pointi 9.

Saimon Msuva- Yanga

Msuva amekuwa mmoja wa wachezaji waliochangia ubingwa katika klabu yake ya Yanga kwa asilimia zote, pamoja na kuwa kinara wa ufungaji bora pia Msuva alionyesha kiwango cha hali ya juu tangu kuanza kwa msimu.

Winga huyo alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Oktoba akishindanishwa na Shiza Kichuya pamoja na Mzamiru Yassin.

Katika mwezi Oktoba ambao ulikuwa na raundi sita, Msuva aliisaidia timu yake kupata jumla ya pointi 14 huku akifunga mabao manne na kutoa pasi tano za mwisho.

John Bocco-Azam

Pamoja na Azam kushindwa kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu huu, nahodha wa Azam FC amekuwa na mchango mkubwa kwa timu yake na ndiye mwamuzi mkubwa wa matokeo waliyopata msimu huu uliomalizika wa ligi kuu.

Bocco ambaye pia ni nahodha wa Azam FC aliwashinda wachezaji wenzake Mzamiru Yasin wa Simba na Said Kipao wa JKT Ruvu kwa mwezi Agosti.

Katika mechi mbili ilizocheza mwezi huo, Bocco aliifungia timu yake mabao matatu likiwamo la kusawazisha dhidi ya African Lyon, pia alifunga mabao mengine mawili kwenye ushindi wa mabao 3-0 wa timu yake dhidi ya Majimaji. Katika mechi hizo mbili, Azam FC ilifanikiwa kupata pointi nne kati ya sita.

Riffat Hamisi- Ndanda FC

Mchezaji Riphat Hamisi wa timu ya Ndanda FC alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Novemba baada ya kuwashinda wenzake Shaban Idd wa Azam FC na Mbaraka Abeid wa Kagera Sugar.

Katika mechi mbili ambazo timu ya Ndanda FC ilicheza kwa mwezi huo, Riphat aliisaidia timu yake kupata ushindi katika michezo yote na kukusanya jumla ya pointi 6 zilizoifanya kushika nafasi ya kumi katika msimamo wa ligi.

Pia aliifungia timu yake mabao mawili katika michezo miwili ambayo timu yake ilicheza kwa mwezi huo.

Source: Dimba
Vinara wa kutoa wachezaji bora wa mwezi Ligi Kuu ya Vodacom [VPL] Vinara wa kutoa wachezaji bora wa mwezi Ligi Kuu ya Vodacom [VPL] Reviewed by Zero Degree on 5/21/2017 06:03:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.