Loading...

Kitendo cha wanawake kutupa watoto baada ya kujifungua chakemewa Zanzibar

Mke wa Rais wa Zanzibar, Mwanamwema Shein
MKE wa Rais wa Zanzibar, Mama Mwanamwema Shein amewataka wanawake kuacha vitendo ya kutupa watoto baada ya kujifungua kwani tabia hiyo ni aibu na kinyume na mafundisho ya dini ya Kiislamu.

Mama Mwanamwema alisema hayo wakati alipofanya ziara katika kituo cha kutunza watoto cha Mazizini kilichopo Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja ambapo katika kipindi cha mwezi mmoja kimepokea watoto 3 waliotupwa na wazazi wao baada ya kujifungua.

Alisikitishwa na tabia hiyo kwa sababu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikichukua juhudi kubwa katika kuimarisha huduma za wajawazito pamoja na uzazi wa mpango. Aliwataka akinamama kutumia dawa zinazotolewa kwa muda wa miezi mitatu bure kwa ajili ya kupunguza kasi ya uzazi.

“Nimesikitishwa sana na tabia iliyojitokeza hivi karibuni ya kutupa watoto na kutishia maisha yao wakati wazazi wanajua kwamba Serikali inatunza watoto hao kwa kuwapatia makazi ya kudumu,” alisema.

Wiki moja iliyopita katika kipindi cha mfungo wa mwezi mtukufu Ramadhani, mtoto wa mwezi mmoja alitupwa katika kituo cha daladala cha Michenzani asubuhi. Naye mke wa Makamu wa Pili wa Rais, Mama Asha Suleiman Iddi aliipongeza Serikali kwa juhudi zake za kutoa matunzo ya watoto pamoja na wazee wasiojiweza katika nyumba zake zilizopo Unguja na Pemba.

Alisema huduma nzuri zinazopatikana katika nyumba hizo hutolewa bure na Serikali kwa kiasi kikubwa zimetoa faraja na kuifanya jamii hiyo kuishi kwa furaha na matumaini makubwa.

Alisema kitendo cha kutupa watoto ni hatari kwani kinaweza kusababisha kifo kwa mtoto na kuwataka kuzitumia nyumba zilizotengwa kwa ajili ya matunzo ya watoto. Katika ziara hiyo wake wa viongozi wakuu wa Serikali walitembelea kituo cha kulea watoto Mazizini pamoja na SOS na kuwatembelea wazee wanaotunzwa hapo Sebleni na Welezo
Kitendo cha wanawake kutupa watoto baada ya kujifungua chakemewa Zanzibar Kitendo cha wanawake kutupa watoto baada ya kujifungua chakemewa Zanzibar Reviewed by Zero Degree on 6/28/2017 11:17:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.