Loading...

Mwigulu Nchemba atoa ufafanuzi juu ya mimba magerezani


BUNGE limeelezwa kuwa ni vigumu mfungwa mwanamke wa kifungo cha muda mrefu kupata mimba akiwa gerezani.

Hayo yalibainishwa jana bungeni na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum (CUF), Raisa Abdallah Mussa.

Mbunge huyo alitaka kujua ni kwanini sehemu ya magereza inayoaminika kama ni sehemu salama, lakini wanawake wanapata mimba wakiwa gerezani.

Akijibu swali hilo, Mwigulu alisema amezunguka katika magereza yote na hakuna eneo ambalo amefika na kukuta mwanamke aliyefungwa kifungo cha muda mrefu amegundulika kuwa na mimba akiwa kwenye kifungo hicho.

“Ni kweli unaweza kukuta wale wenye kifungo cha muda mfupi wakajifungua wakiwa gerezani, lakini kujifungua wakiwa gerezani haina maana kuwa mimba kaipatia gerezani,” alisema Mwigulu. 

Alibainisha kutokana na sheria kali za majeshi likiwamo Jeshi la Magereza, haitawezekana mwanamke mfungwa apate mimba akiwa ndani ya gereza halafu taarifa zikafichwa.

Katika swali la msingi, Mbunge huyo alitaka kujua serikali imejipanga vipi katika kuwanusuru watoto ambao wanawake wamekuwa wakijifungua wakiwa magerezani.

“Je, serikali haioni kuwa inavunja haki za binadamu kwa kuwaweka magerezani watoto hao wasio na makosa, na je, inaweza kulipa Bunge takwimu za wanawake waliokinzana na sheria na kufungwa kwa miaka mitano iliyopita?” alihoji. 

Akijibu swali hilo la msingi, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yusuf Masauni, alisema kwa muda wa miaka mitano jumla ya wanawake 2,008 walikinzana na sheria na kufungwa magerezani.

Aidha, alisema kwa watoto kuwapo magerezani na wazazi wao ni kutokana na sheria ya mtoto ya kutaka mtoto kupata haki yake ya kunyonya maziwa ya mama.
Mwigulu Nchemba atoa ufafanuzi juu ya mimba magerezani Mwigulu Nchemba atoa ufafanuzi juu ya mimba magerezani Reviewed by Zero Degree on 6/21/2017 11:08:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.