Loading...

Wakurugenzi wapewa siku 7 kulipa stahiki za walimu wapya wa sayansi


WAKURUGENZI wa Halmashari zilizopokea walimu wapya wa Sayansi, Hisabati na wataalamu wa maabara za nchini wameagizwa kuhakikisha wanalipa stahiki za watumishi hao ndani ya siku saba.

Agizo hilo lilitolewa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angela Kairuki, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Ukerewe (Chadema), Joseph Mkundi. 

Mkundi alitaka kujua kauli ya serikali kwa kuwa mwanzoni mwa mwaka huu ilisambaza walimu hasa wa sayansi, lakini kumekuwapo na malalamiko mengi yawalimu hao kuishi katika mazingira magumu kwa sababu ya kutolipwa stahiki zao.

Akijibu swali hilo, Kairuki alisema ni jambo la kusikitisha watumishi hao kutolipwa stahiki zao hasa ikizingatiwa halmashauri moja imepangiwa walimu 12.

“Inakuwaje halmashauri inashindwa kuwahudumia watumishi wake wapya waliopangiwa kituo kwa mara ya kwanza, nitumie hadhara hii kuziagiza Halmashauri zilizopokea walimu hawa na wataalamu wa maabara za sayansi zihakikishe ndani ya siku saba zimewalipa stahiki zao zote,” alisema Kairuki. 

Katika swali la msingi, Mkundi alitaka kujua serikali ina mpango gani wa kutoa posho ya mazingira magumu kwa watumishi wa maeneo ya pembezoni ikiwamo Wilaya ya Ukerewe.

Akijibu swali hilo, Kairuki alikiri kuwa watumishi walioko katika Halmashauri zilizo katika maeneo ya pembezoni ikiwamo Wilaya hiyo hufanya kazi katika mazingira magumu na upungufu mkubwa wa watumishi.

Alisema mwaka 2010 serikali ilipitisha Sera ya Malipo ya mishahara na Motisha katika Utumishi wa Umma ambayo miongoni mwa malengo yake mahsusi ni kuwavutia, kuwapa motisha na kuwabakiza watumishi katika utumishi wa umma, hivyo kupunguza tatizo la uhaba wa watumishi.

Alibainisha katika kutekeleza sera hiyo mwaka 2012/13, Halmashauri 33 za Wilaya ikiwamo Halmashauri ya Ukerewe ziliwezeshwa kuandaa miongozo ya kutoa motisha kwa watumishi.

Kutokana na zoezi hilo, alisema Halmashauri 29 ziliandaa na kuwasilisha katika ofisi yake miongozo iliyobainisha aina za motisha zinazohitajika kwa ajili ya watumishi wake.

“Utekelezaji wa miongozo hiyo kwa Halmashauri zote 29 ulikadiriwa kugharimu jumla ya Sh. bilioni 331.087 kwa mwaka ambapo kati ya hizo kiasi cha Sh. bilioni 314.372 kilihitajika kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kiasi cha Sh. bilioni 16.716 kilihitajika kwa ajili ya matumizi,” alisema Kairuki. 

Hata hivyo alisema utekelezaji wa miongozo hiyo haujaanza kutokana na ufinyu wa bajeti ya serikali.
Wakurugenzi wapewa siku 7 kulipa stahiki za walimu wapya wa sayansi Wakurugenzi wapewa siku 7 kulipa stahiki za walimu wapya wa sayansi Reviewed by Zero Degree on 6/30/2017 10:32:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.